Profesa Kamuzora :UTT AMIS Wawekezaji wananufaika ipasavyo na uwekezaji
Imeelezwa kuwa uwekezaji kupitia UTT-AMIS ni rahisi na unamuwezesha mwananchi wa kawaida kushiriki kikamilifu katika sekta ya fedha, ambapo mwekezaji huweka fedha zake na taasisi hiyo hufanya kazi ya kuzisimamia na kuziwekeza kitaalamu kwa lengo la kuzalisha faida.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa UTT-AMIS, Profesa Faustin Rweshabura Kamuzora, amesema taasisi za uwekezaji katika sekta ya fedha zina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi, huku UTT-AMIS ikiendelea kujiimarisha ili kuongeza thamani ya uwekezaji kwa Watanzania.
" UTT-AMIS inaendelea kujikita zaidi katika eneo la usimamizi wa mali (wealth management) ili kuhakikisha wawekezaji wananufaika ipasavyo na uwekezaji wao, sambamba na kuimarisha imani ya umma katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja," amesema Profesa Kamuzora.
Profesa Kamuzora ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wawekezaji wa Mfuko wa Umoja, uliofanyika kwa lengo la kujadili mwenendo wa mfuko huo, mafanikio yaliyopatikana pamoja na mwelekeo wa uwekezaji kwa miaka ijayo.
Amesema UTT-AMIS kwa sasa ina jumla ya mifuko saba ya uwekezaji, na imejipanga kuongeza tija na mazao ya mifuko hiyo kwa lengo la kufanikisha faida kwa wawekezaji wake.
Ameongeza kuwa kwa sasa UTT-AMIS ina zaidi ya wawekezaji 500,000, ambapo zaidi ya nusu ya wawekezaji wote katika sekta ya fedha nchini wanahudumiwa na taasisi hiyo, hali inayoonesha ukubwa na mchango wake katika maendeleo ya soko la mitaji nchini.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa UTT-AMIS, Bw. Simon Migangala, amesema taasisi hiyo imeendelea kuonesha ukuaji mzuri, hususan kupitia Mfuko wa Umoja, ambao kwa sasa umefikia thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 400, huku ukiendelea kukua kwa wastani wa asilimia tatu, wakati mifuko mingine ikikua kwa wastani wa asilimia mbili.
Bw. Migangala amesema mwaka 2024 thamani ya jumla ya mifuko ya UTT-AMIS ilikuwa shilingi trilioni 2.2, lakini hadi mwaka huu imeongezeka na kufikia zaidi ya shilingi trilioni 3.3, ongezeko linalotokana na kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wawekezaji.
Ameongeza kuwa idadi ya wawekezaji imeongezeka kwa kasi, ambapo mwaka jana kulikuwa na wawekezaji takribani 320,000, huku mwaka huu pekee ikishuhudiwa ongezeko la wawekezaji wapya zaidi ya 140,000.
Vile vile imeelezwa kuwa UTT AMIS inaendelea kutumia mbinu na njia mbalimbali za kisasa ili kuwawezesha wawekezaji wa makundi yote kuwekeza katika mifuko tofauti kulingana na uwezo na malengo yao ya kifedha.
Kwa ujumla, taasisi hiyo imeahidi kuendelea kuchukua hatua za kuvutia wawekezaji wengi zaidi, kuimarisha elimu ya uwekezaji kwa umma, na kuchangia kikamilifu katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla

Post a Comment