Ads

AZIMIO LA MUSOMA NA JULIUS NYERERE


Judith Mhina
Mwambawahabari
Ni miaka 17 sasa tangu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipoaga dunia. Katika kuadhimisha kumbukumbu ya Mwalimu Idara ya Habari Maelezo ilipata fursa ya kufanya mahojiano na Dkt Fidelice Mafumiko Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ambaye alikuwa ni kati vijana walioguswa na utekelezaji wa Azimio la Musoma na pia wahitimu wa mafunzo ya ualimu walioandaliwa kwa ajili ya kukabiliana na uhaba wa walimu wa sayansi katika shule za sekondari kupita mafunzo yaliyojumuisha kidato cha tano na sita pamoja na ualimu katika muda wa miaka mitatu.
Dkt. Mafumiko leo anaeleza hali halisi katika kampeni ya kupata walimu wa masomo ya sayansi kwa kutumia mfumo wa kuunganisha “A-level na mafunzo ya ualimu kwa miaka mitatu, yaani miwili ya kidato cha tano na sita, na mmoja wa mafunzo ya ualimu. Vile vile atatueleza kama bado AZIMIO LA MUSOMA lina nafasi kwa sasa?
Dr.Mafumiko-1(1)  SIZE 640-480
Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Dkt Fidelice Mafumiko
Swali:
Tueleze historia fupi ya Azimio la Musoma mahusiano yake na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere?
Jibu:
Ndugu Mwandishi, huwezi kuzungumzia Azimio la Musoma bila kumtaja Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa sababu yeye ndiyo alikuwa mwasisi wa azimio hilo. Pia ni azimio ambalo lilitia mkazo kuondokana na adui ujinga  ambaye ni kati ya maadui watatu wakiwemo Maradhi na Umasikini.
Historia ya Azimio la Musoma inaanzia pale chama tawala wakati huo TANU kuorodhesha kuwa ni miongoni wa ahadi kumi za mwana-TANU ambapo ilikuwa ni kupambana na kuwashinda adui umaskini, maradhi na ujinga. Katika mapambano hayo, Mwalimu Nyerere alitambua kuwa kwa kutokomeza maadui hao watatu, watanzania wangepata nafasi ya kuendeleza taifa lao kisiasa, kijamii na kiuchumi, ambapo suala hilo limepewa kipaumbele zaidi katika uongozi wa awamu ya Tano wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.

Azimio hilo la Musoma la mwaka 1974 liliweka mkazo kuhusu elimu ya msingi kwa wote, uchangiaji wa elimu ya juu na  kufanya kazi kabla ya kujiunga na chuo kikuu baada ya kuhitimu kidato cha sita. Upande wa   wahitimu wa kidato cha sita wasichana walioruhusiwa kujiunga vyuo vikuu moja kwa moja, mara tu wamalizapo mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa - JKT.
Elimu ililenga kumkomboa mtu kifikra na ilimaanisha kujifunza na kuthamini kazi, kwa hiyo dhana ya kazi ilikuwa sehemu ya mafunzo katika vituo vyote vinavyotoa elimu zikiwemo shule za sekondari. Dhana hiyo haina tofauti na dhana ya sasa ya HAPA KAZI TU kwa kujifunza au kufunzwa.
Mwalimu Nyerere alisisitiza dhana ya elimu kwa wote kwa kuzingatia mahitaji ya watu wa rika zote. Kwake yeye elimumsingi ilimaanisha maendeleo ya watu katika kuyaelewa, kutafsiri na kuyaendeleza mazingira yao. Hivyo basi dhana hiyo ilisababisha mfumo wa elimu kuzingatia ubora wa elimu ya shule za msingi/sekondari na elimu ya watu wazima.
Swali:
Kwa kuwa wewe ulikuwa mmoja wa zao la utekelezaji wa Azimio la Musoma, unadhani lilikuwa na manufaa kwenu au nini mmejifunza kutokana na Azimio hilo?
Jibu
Hakika ninaweza kusema mimi kama mmojawapo wa watu waliopitia Azimio la Musoma, Azimio hili lilikuwa lina manufaa si kwa tuliolitekekeza tu bali kwa watanzania wote.

Mosi, nilijifunza kuwa kama muhitimu wa kidato cha sita na stashahada ya ualimu katika sayansi na hisabati, kupitia Azimio hili, kabla ya kujiunga na elimu ya chuo kikuu, tulichangia kwa kufundisha katika shule mbalimbali za sekondari, kuhamasisha vijana katika shule za sekondari kupenda masomo ya sayansi na kutatua kero kubwa ya uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi iliyokuwepo wakati huo. Hakika katika hili niliona ni umuhimu wa kutumia maarifa na ujuzi nilioupata kwa kuwapa elimu watu wengine waliokuwa na kiu kubwa ya kupata elimu ya sekondari;
Pili, kupitia Azimio la Musoma kusisitiza elimu ya msingi kwa wote, kiwango cha adui ujinga kilipungua na elimu ya watu wazima ilihusishwa na elimu ya kujitegemea na maisha ya kila siku; na
Tatu, tuliandaliwa kuthamini kazi na kuwa wazalendo kwa nchi yetu kwa kutanguliza maslahi ya Taifa.
Swali:
Unadhani operesheni/kampeni kama hiyo inahitajika kwa sasa kutokana na upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi nchini?
Jibu:
Kila zama na kitabu chake na ikumbukwe kuwa kipindi hicho uhaba wa walimu wa masomo karibu yote ulikuwa ni mkubwa sana. Kutokana na uchanga wa Taifa letu hasa mahitaji wa kuwa na wataalamu wetu wazalendo.
Vilelvile, kipindi hicho cha Azimio la Musoma, Mwalimu Nyerere kwa kutambua umuhimu wa kuwa na walimu watakaokabili ongezeko la wanafunzi mashuleni, licha ya mfumo wa kuandaa walimu wa sekondari wa “ Mtindo wa Mkwawa – Mkwawa Model”alianzisha mfumo wa kuandaa walimu ambao walipata mafunzo ya daraja C, maarufu kama walimu wa “Universal Primary Education-UPE”.  Kwa muda mfupi Tanzania ilijikuta inaziba pengo la walimu mashuleni kwa ngazi zote.
Kwa sasa serikali imefanya maboresho makubwa katika sekta ya elimu, kwanza upande wa uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi, serikali imeweka mipango mbalimbali ikiwepo kuweka kipaumbele kwa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi, ili kutoa motisha ya wanafunzi kusoma masomo hayo.  
Hivyo kupitia sera ya serikali kugharimia mafunzo ya sayansi na elimu katika vyuo vikuu itaweza kuandaa walimu wengi na watalamu wengine kwa kada ya sayansi na masomo yanayohusiana na hayo kama vile kilimo, uhandisi, na ufamasia. Ni imani yangu pia mkazo huu utasaidia kujiandaa kuelekea Tanzania ya Viwanda, iliyowekewa dira na serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Mhe. Dkt, John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Swali:
Ni faida gani uliyoipata katika kukujenga kitaaluma na kiutendaji wa kazi kwa kupitia ngazi mbali mbali za kazi hadi sasa?
Jibu:
Binafsi nimejengeka kitaaluma na kiweledi kama mwalimu wa sayansi na mtafiti katika masuala ya ufundishaji wa somo la kemia pamoja uthibiti ubora katika ujifunzaji na ufundishaji kwa ujumla. Kwa kupitia mafunzo kazini ya muda mfupi na mrefu nimeweza kujiendeleza kitaaluma hadi kufikia kiwango cha shahada ya Uzamivu.
Kiutendaji nimepata uzoefu kwa kufundisha, kufanya utafiti na ushauri wa kitaalamu katika makundi mbalimbali ya kijamii. Lakini hatua kubwa kwangu pia ni kukua katika uongozi na kuaminiwa na mamlaka husika kuniteua kuwa Mkurugenzi /Mtendaji Mkuu wa Taasisi hii ya Elimu ya Watu Wazima.
Kwa kuwa Mkurugenzi pamoja na kuwa ni muda mfupi karibu miaka miwili sasa, nimepata uelewa zaidi kwa mambo ya elimu ya watu wazima na fursa za elimu kwa vijana na watu wazima kupitia ujifunzaji Huria na Masafa. Hivyo kuna mambo nimejifunza hapa TEWW ambayo, nisingeipata kamwe kwa kuwa mwalimu darasani au mhadhiri.
Swali:
Mkurugenzi wewe ndio mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima - TEWW.  Je ni nini hasa mnachojishughulisha nacho? Elimu ya Watu Wazima bado ni Elimu ya ngumbaro kama ilivyotambulika enzi za Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere?
Jibu:
Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ilianzishwa mwaka 1960 kama sehemu ya kitengo cha mafunzo ya ziada cha Chuo Kikuu cha Makerere, Kampala Uganda, chini ya Chuo kikuu cha London. Mwaka 1963 Taasisi ikawa Idara ya Elimu ya Watu Wazima chini ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Taasisi iliendelea kukua na kupata hadhi na kuwa Taasisi inayojitegemea chini ya Wizara ya Elimu kwa wakti huo kupitia Sheria ya Bunge Namba. 12 ya mwaka 1975.
Elimu ya ngumbaru ilimaanisha madarasa ya kisomo yaani kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu. Lakini Elimu ya Watu Wazima (EWW) ni dhana pana sana, ambayo inahusisha kisomo chenye manufaa, yaani kutumia stadi za kisomo katika kujiletea maendeleo katika nyanja mbalimbali za maisha.
Pia Elimu ya Watu Wazima inahusisha elimu ya kujiendeleza katika ngazi mbalimbali za kielimu, elimu ya wafanyakazi ili kuboresha utendaji mahala pa kazi, elimu kwa umma juu ya masuala mtambuka ya maendeleo, na mengine zaidi..
Kwa wakati huo Mwalimu Nyerere alisisitiza kuwa kusoma, kuandika na kuhesabu ni njia tu ya kumwezesha mtu awe na uwezo wa kupata taarifa ili aweze kufahamu vitu mbalimbali katika jamii yake ili aweze kuondokana na ujinga, maradhi na umaskini. Ndio maana kulikuwa na kitabu cha kilimo cha pamba Mwanza kwa watu wa Mwanza na vitabu vya kilimo cha mahindi kutokana na uhitaji wa maeneo tofauti, hivyo haikuwa elimu ya ngumbaro kama watu walivyokuwa wanatafsiri, lakini ilikuwa ni elimu inayohusisha na mazingira ya mtanzania ili aweze kumudu mazingira yake.
Majukumu au kazi za TEWW, kadiri ya sheria iliyoiunda ni nyingi, ila kwa ufupi shughuli hizo zimejikita katika utekelezaji wa majukumu yafuatayo:-
Kutoa mafunzo ya Elimu ya Watu Wazima kwa kuandaa wataalamu, wawezeshaji na wasimamizi wa Elimu ya Watu Wazima na elimu ya kujiendeleza nje ya Mfumo rasmi, ambapo hujumuisha uenaendeshaji wa programu za Astashahada, stashahada na shahada katika Elimu ya Watu Wazima na Mafunzo Endelevu, Elimu ya Watu Wazima na Maendeleo ya Jamii, uandishi wa habari na elimu kwa umma.
Kutoa elimu kwa umma juu ya masuala muhimu ya kitaifa na mtambuka yakiwemo afya, uraia mwema, utunzaji wa mazingira, lishe bora na haki za binadamu. Kwa mfano mradi unaoendelea wa kuzuia ndoa za utotoni za kulazimishwa, mradi wa mimba za utotoni, kuandaa zana kuhamashisha jamii kama kuandaa video inayohamasisha kujiunga na kisomo, yaani kusoma, kuandika na kuhesabu, pamoja na majarida ya wanawake kuhusiana na masuala ya jinsia.
Kufanya utafiti juu ya masuala ya elimu ya watu wazima na elimu katika mfumo usio rasmi na kusambaza matokeo ya utafiti huo kwa mipango endelevu ya elimu ya watu wazima na jamii.
Kutoa ushauri wa kitaalamu kwa serikali, taasisi nyingine na mashirika yasiyo ya kiserikali kuhusu mitaala na uandaaji wa vitabu na majarida ya elimu ya watu wazima na elimu ya kujiendeleza nje ya mfumo usio rasmi wa elimu kwa vijana na watu wazima wenye uhitaji.
Aidha, tunatoa ushauri katika elimu changamani baada ya msingi Integrated Post-Primary Education kwa kutoa mafunzo ya kuandaa mitaala, zana za kujifunzia moduli na za kufundishia katika mfumo huria pamoja na kufanya tathmini.
Kutoa na kuratibu elimu ya sekondari kwa njia ya Ujifunzaji Huria na Masafa yaani “Open and Distance Learning” kwa ajili ya vijana nje ya shule na watu wazima wenye uhitaji na waliokosa elimu hiyo.
Swali:
Watafiti na waalimu kwa sasa wanatafuta mbinu mbalimbali za kupunguza au kuondoa kabisa idadi ya wasiojua kusoma na kuandika unadhani iko haja ya kurudia mbinu za Baba wa Taifa? Rejea gazeti la The Guardian la tarehe 22 Septemba 2016 ukurasa wa 5
Jibu:
Ni kweli kabisa watafiti na waalimu wanafanya mbinu mbalimbali ili kupunguza idadi ya wasiojua kusoma, kimsingi katika sensa ya 2012 ilionesha asilimia 22 walikuwa hawajui kusoma na kuandika. Lakini sisi kama Taasisi tunachangia katika kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuandaa na kutumia wanachuo kufundisha katika vituo vya kisomo ili kupunguza uhaba wa walimu wa kisomo na pia kuunganisha mafunzo ya nadharia na vitendo.
Pia tumefufua programu za Astashahada ya elimu ya watu wazima na mtaala wake umeboreshwa au kudurusiwa kulingana na mahitaji katika jamii, ili kuwezesha kuandaa wawezeshaji/walimu mahiri wa madarasa ya kisomo. Taasisi inazalisha wasomi wengi katika sekta, fani, ambazo tuaamini kuwa wanaweza kuwafikia wananchi wengi hata vijijini endapo watapata fursa ya kuajiriwa.
Aidha, katika kuondokana/ kupunguza tatizo hilo serikali imefanya maboresho makubwa katika elimu ya msingi kwa kupitia sera ya elimu na mafunzo ya 2014. Ambapo zile stadi tatu za kusoma, kuandika na kuhesabu zimetiliwa mkazo na mtaala huo mpya umeanza na walimu wa shule za msingi wamepewa hayo mafunzo.  
Hata hivyo, haya peke yake hayatoshi, kwani kunahitajika nguvu ya pamoja kuweza kukabili tatizo hili. Mwalimu Nyerere alikuwa na utashi mkubwa sana wa kisiasa na alithamini sana mchango wa elimu ya Watu wazima katika kufikia maendeleo ya haraka. Ni muhimu hata sasa kila mdau aone haja ya kuchangia harakati za kufuta ujinga angalau taifa lizidi hata ile asilimia iliyofikiwa miaka ya 1980 ya kuwa asilimia 90 wa watu wenye stadi za KKK.
Swali:
Nini nafasi yenu katika suala hilo kama Taasisi?
Jibu
Jukumu la taasisi ni kuendelea kubuni na kuandaa mipango ya kielimu yenye lengo la kuwezesha jamii kupenda kujifunza masuala ya maendeleo. Hivyo kuleta mabadiliko chanya katika mazingira ya watu na jamii inayowazunguka.
Hii maana yake ni kwa TEWW kuendelea kuandaa program mtambuka za mafunzo kwa vijana nje ya shule na watu wazima wenye kuhitaji kupata maarifa na ujuzi mbalimbali ikiwemo stadi KKK. Kuendelea kufanya tafiti katika eneo la Elimu ya Watu Wazima na  elimu katika mfumo usio rasmi ili kubaini ni changamoto zipi zinazopelekea watu kutokujua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Kuendelea kutoa mafunzo ya elimu ya watu wazima kwa kuandaa wataalamu, wawezeshaji na waratibu wa Elimu ya watu wazima ili wawe na uwezo wa kutengeneza madarasa ya kisomo katika maeneo yao waliyotoka.
Kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kujua kusoma, kuandika na kuhesabu ili kuongeza tija katika kazi ambazo wanazifanya katika jamii yao, mfano uvuvi, ufundi na uhunzi.
Swali:
Una wito wowote kuhusiana na Azimio la Musoma kwa watanzania na Vijana wetu kwa ujumla?
Jibu:
Ndugu mwandishi wewe mwenyewe ni shahidi kuwa ni vigumu sana kuiongozi jamii ya wajinga, pia wasioelewa mazingira yao hivyo ninatoa wito wa wanajamii wote, viongozi katika ngazi mbalimbali kuweka mipango ya Elimu ya Watu Wazima ili kujenga jamii inayopenda kujifunza na kutafuta taarifa na hivyo kuyaelewa mazingira yao ili waweze kuyatawala na kuyabadilisha kwa maendeleo endelevu ya taifa letu.

No comments