Borega: TFC Inawasaidia Wakulima Kupata Matumizi Bora ya Mbolea
Na Francisco Peter, Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Uendeshaji Biashara wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Lameck Borega, amesema kuwa uthibiti wa mbolea unatokana na ukweli kwamba wakala yeyote wa mbolea lazima awe amepitia mafunzo yanayotolewa na mamlaka husika.
Amesema ni lazima wakala apate mafunzo ya uthibiti bora wa mbolea pamoja na namna ya kuwaelimisha wakulima juu ya matumizi sahihi ya mbolea.
Akizungumzia upatikanaji wa mbolea bora kwa wakulima, Borega amesema mawakala wao ni walimu wazuri wa matumizi ya mbolea, hali inayowasaidia wakulima kupata mazao bora.
“Ikiwa mbolea inatolewa kwa ruzuku ya serikali, wale wanaouza kwa bei tofauti na bei ya ruzuku wanapaswa kuacha mara moja, kwa sababu mwisho wa siku watakamatwa,” alisema Borega.
Ameeleza kuwa mbolea zote za serikali zina namba maalumu, sambamba na wakulima ambao nao wana namba za utambulisho.
Kupitia namba hizo, mamlaka husika zinaweza kumtambua mkulima na kuhakikisha zoezi la usambazaji wa mbolea linafanyika kwa uwazi na usafi.
Aidha, Mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa wanaofanya kinyume na maagizo ya serikali wanaweza kuchukuliwa hatua za kisheria, kwani vitendo hivyo vinakwaza juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo kwa wakati na kwa bei nafuu.
Katika miezi kadhaa iliyopita, TFC kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Uendeshaji Biashara, Lameck Borega, imekuwa ikitembelea wakulima katika maeneo mbalimbali, yakiwemo kata za Mang’ola, Baray, Endamanga na Jobaji, zilizopo katika Bonde la Ziwa Eyasi, Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.
Ziara hizo zimelenga kujionea hali halisi ya usambazaji wa mbolea, kufuatilia utekelezaji wa mpango wa ruzuku, pamoja na kubaini mahitaji halisi ya mbolea kwa wakulima.
Bonde la Ziwa Eyasi linajulikana kwa uzalishaji wa mazao kama vitunguu, mahindi, maharage na mpunga. Eneo hilo lina zaidi ya hekta 8,000 za skimu za umwagiliaji, na ni miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa za kilimo nchini.

Post a Comment