Ads

RC CHALAMILA KUHUSU UTEKAJI , MAUAJI YA WATOTO DAR.

  

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amezungumzia matukio ya mauaji na utekaji wa watoto jijini humo akikiri kuwa yapo lakini si kama yanavyoripotiwa.

Kauli hiyo inafuatia taarifa zinazoenea na kuleta taharuki kuhusu matukio ya watoto kupotea, kutekwa na kuuawa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwamo Dar es Salaam.

Akizungumzia matukio hayo leo, Julai 26, 2024, katika kipindi cha Good Morning cha Wasafi FM, Chalamila amesema si kama Dar es Salaam haijawahi kupata majanga hayo, imeshawahi, lakini mengi yanapofuatiliwa wanakuta si ya kweli.

Ingawa Chalamila amekiri kuwepo tukio la kifo cha utata cha mtoto alichosema kilitokea Temeke, amesema bado wanaendelea na uchunguzi.

"Hali haipo hivyo inavyotamkwa," amesema Chalamila, akitaja baadhi ya matukio yaliyozua taharuki.

“Jana Chamazi kulikuwa na taharuki ikidaiwa watoto wawili wametekwa na watu waliokuwa kwenye gari aina ya Noah, walipofuatilia tukio hilo, vijana hao walikuwa ni wanafunzi watoro shuleni, hivyo wakatafuta njia watakavyorudi kusema nyumbani, wakaona watumie mbinu ya kusema walitekwa. Tulipowafuatilia zaidi wakasema hawakutekwa, walikuwa ni watoro shuleni, huo ni mfano wa kwanza.

“Wiki iliyopita kule Temeke, watoto walikuwa wakioga, mmoja aliyekuwa amevua nguo na kuziweka pembeni aliondoka kwenda nyumbani bila nguo zake. Tukio hilo lilisababisha taharuki, ikidaiwa yule mtoto amechinjwa kumbe aliondoka na kuacha nguo zake eneo alipokuwa akioga.

"Amesema tukio jingine ni hukohuko Temeke ambako alitokea mama mmoja amevaa hijabu, akawa anamuuliza mtoto amwelekeze njia.

“Amesema mama huyo ni kiziwi, wakati akielekezwa, kuna mama yake alikuwa anaangalia dirishani akapiga kelele kuwa yule mama anamteka mtoto, watu wakajaa wakampiga na ilipofuatiliwa yule mama kumbe ni kiziwi na aliomba kuelekezwa njia na si vinginevyo.

"Chalamila amesema katika taharuki hizo kuna watu wanachukua pia habari za matukio yaliyopita na kuzirudisha, jambo ambalo nalo linaibua sintofahamu inayoendelea jijini Dar es Salaam." Amesema.

No comments