Ads

MHE. KAIRUKI ATOA MAAGIZO 14 TANAPA

Na. Edmund Salaho/TANAPA

Waziri mwenye dhamana ya Maliasili na Utalii nchini Mhe. Angellah Kairuki (Mb), ameongoza kiapo cha utii kwa Kamishina wa Uhifadhi - TANAPA, Musa Nassoro Kuji Juma katika hafla ya uapisho iliyofanyika leo makao makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania, jijini, Arusha.

Akizungumza baada ya uapisho huo Waziri wa Maliasili na Utalii alitoa maagizo 14 kwa Kamishna wa Uhifadhi Kuji ikiwemo kuhakikisha ulinzi wa maliasili unaimarishwa wakati wote, kusimamia na kufuatilia doria zifanyike ipasavyo ili kukabiliana na vitendo visivyofaa ndani ya Hifadhi Ikiwemo swala la Mifugo, na uchimbaji wa madini.

“Endelea kuhakikisha kuwa hifadhi zinaendelea kuimarika, kukusanya mapato lakini hifadhi zingine ziendelee kufanya vizuri kama ambavyo Serengeti inafanya vizuri, nunueni vitendea kazi na kuboresha maslahi ya watumishi pamoja na kuendelea kujikita kutangaza utalii kwa kushirikiana na taasisi zingine kama TTB” Alisema Mhe.Kairuki.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt.Hassan Abbas alisisitiza kufanya kazi kama timu na kubainisha kuwa kila nafasi inakuja na majukumu yake.

“Nafasi hizi zinakuja na majukumu yake, “Team work” ni muhimu sana. Nikuhusie sana, TANAPA ni taasisi kubwa sana nchini na duniani, shirikianeni na sisi wizara tutakuwa tayari kushirikiana na wewe. Mtegemee Mwenyezi Mungu katika majukumu yako ”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini -TANAPA, Jenerali (Mstaafu) George Waitara alimpongeza Kamishna Kuji kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Kamishna wa Uhifadhi TANAPA.

“Binafsi sina mashaka na uzoefu wako ndani shirika wa miaka 33 ni matumaini yangu uzoefu huo utatumia katika kukuza uhifadhi na utalii katika shirika na kuendelea kufanya vizuri katika ngazi za kimataifa”.

Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA Mussa Nassoro Kuji Juma ameahidi ushirikiano na watumishi wote kuhakikisha wanalinda urithi wa maliasili zilizopo nchini sambamba na kufanya kazi kwa bidii na nidhamu.

“Awali ya yote namshukuru Mungu kwa tukio hili la kuvishwa vyeo, pili nimshukuru Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniteua kuwa Kaimu Kamishna na baadae kuwa Kamishna wa uhifadhi wa TANAPA “ alisema Kamishna Kuji.

Aidha, Kamishna Kuji alisisitiza ushirikiano kwa watumishi ili kufikia adhma ya serikali ya kuanzisha taasisi hii na kuahidi kusimamia maeneo yote ya hifadhi kikamilifu.

“Mimi na watumishi wenzangu kwa kushirikiana na bodi ya wadhamini tutaendelea kusimamia kikamilifu maeneo ya Hifadhi wakati wote tutajitahidi kutumia taaluma,uzoefu,busara, na kumtanguliza Mungu katika kuhakikisha Rasilimali zote zilizopo katika Hifadhi za Taifa zinahifadhiwa kikamilifu”

Kamishna Musa Nassoro Kuji Juma amechukua nafasi ya Kamishna wa TANAPA, William Mwakilema ambaye sasa ameteuliwa na Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa wilaya ya Korogwe.

No comments