Ads

TARURA KUJENGA DARAJA LA KUDUMU KILOSA KUDHIBITI MVUA.

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inatarajia kuanza usanifu wa daraja la kudumu la chuma (Mabey Bridge) litakalojengwa ili kuunganisha vijiji vya Nyali na Nzumbo katika kata ya Ulaya-Mikumi Wilayani Kilosa.

Hatua hiyo inakuja baada ya daraja la awali kusombwa na maji kufatia mvua kubwa iliyonyesha Mkoani Morogoro hivi karibuni na kusababisha wananchi kukosa huduma muhimu ikiwemo miundombinu ya barabara.

Akizungumza leo Januari 29, 2024 akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua hali y miundombinu ya barabara, Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff, amesema kuwa atawatuma wataalamu wa TARURA kutoka Makao Makuu kwa ajili kufanya usanifu wa ujenzi wa daraja la kudumu la chuma ili kuunganisha vijiji hivi vya Nyali na Nzumbo.


 Pamoja na hilo, amemwelekeza Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro kuanza mara moja ujenzi wa daraja la watembea kwa miguu (Kiteputepu) ili wananchi wa vijiji hivyo waendelee kupata huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Mbunge wa Jimbo la Mikumi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge - TAMISEMI Mhe. Dennis Londo amesema barabara nyingi za Jimbo la Mikumi zimeharibika vibaya kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kuiomba TARURA kuangalia uwezekano wa kukarabati.

Hata hivyo Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Ladislaus Chang'a wakati akitoa utabiri wa Mvua za Msimu Novemba 2023 hadi April 2024, alisema kuwa kuwa miundombinu ya usafiri na usafirishaji inaweza kuathirika hususan maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Juu ya Wastani. 

Alisema kuwa matukio ya hali mbaya ya hewa yanaweza kuharibu miundombinu ya barabara, ongezeko la ajali barabarani katika usafiri wa nchi kavu (barabara na reli); kuchelewa au kusitishwa kwa safari.

Aliwashauri wadau wa sekta ya miundombinu ya barabara kuchukua hatua stahiki katika utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu mbalimbali pamoja na ukaguzi wa mara kwa mara wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

No comments