Ads

MVUA YALETA HASARA YA BILIONI 65 TARURA.

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), imesema inahitaji shillingi bilioni 65.1 ikiwa ni fedha ya dharura kwa ajili ya ukarabati wa barabara na madaraja yaliyoharibika kwa mvua.

Akizungumza leo Januari 24, 2024 Jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na Menejimenti ya TARURA, Makatibu Tawala Wasaidizi Miundombinu, Makandarasi wazawa, Wataalamu washauri na Taasisi za kibenki, kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere , Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff, amesema kuwa amesema tathmini ya uharibiu wa miundombinu ya barabara uliosababishwa na mvua imefanyika kuanzia mwezi Juni 2023 hadi Desemba 2023 ikijumuisha halmashauri 184.

Amesema tathmini hiyo inaonesha kuwa kiasi cha zaidi ya sh bilioni 33.124 zinahitajika kwa ajili ya marekebisho ya miundombinu ya barabara iliyoathirika na mvua kwenye halmashauri 153.

Amesema, inakisiwa jumla ya sh bilioni 32 zinahitajika kati ya Januari hadi Juni 2024 ikiwa ni fedha za tahadhari kwa ajili ya uharibifu wa mvua hadi msimu utakapoisha mwezi Juni, 2024.

“Hivyo kulingana na tathmini hiyo na makisio hadi msimu wa mvua utakapoisha jumla ya Sh bilioni 65.100 zinahitajika kama fedha za tahadhari, kwa kuwa sh bilioni 21.460 zimeshatengwa kutakuwa na nakisi ya sh bilioni 42.640,” amesema.

Hata hivyo Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Ladislaus Chang'a wakati akitoa utabiri wa Mvua za Msimu Novemba 2023 hadi April 2024, alisema kuwa kuwa miundombinu ya usafiri na usafirishaji inaweza kuathirika hususan maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Juu ya Wastani. 

Alisema kuwa matukio ya hali mbaya ya hewa yanaweza kuharibu miundombinu ya barabara na reli, ongezeko la ajali barabarani katika usafiri wa nchi kavu (barabara na reli); kuchelewa au kusitishwa kwa safari.

Aliwashauri wadau wa sekta ya miundombinu ya barabara kuchukua hatua stahiki katika utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu mbalimbali pamoja na ukaguzi wa mara kwa mara wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

No comments