MVUA DAR ZAMSTUA NAIBU WAZIRI WA UJENZI
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya ameuagiza Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kufanya kazi usiku na mchana ili kurejesha mawasiliano ya miundombinu ya Barabara na madaraja yalioathiriwa na mvua kubwa iliyonyesha juzi jijini Dar es Salaam.
Waziri Kasekenya ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam wakati akikagua miundombinu ya madaraja na Barabara zilizoathiriwa na mvua katika wilaya za Ilala na Kinondoni ambapo ameipongeza TANROADS kwa kufanikiwa kurudisha mawasiliano ya barabara ya Mbuyuni Kunduchi hadi Ununio ambayo ilikuwa haipitiki.
Waziri Kasekenya amesema Serikali imejipanga ipasavyo kukabiliana na changamoto zitakazosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini na kuwataka wananchi kutoa ushirikianao kwa TANROADS ili kuepuka madhara katika msimu huu wa mvua.
"TANROADS hakikisheni kwamba daraja hili linamazika kupitika pande zote mbili na kuweka kingo imara na alama elekezi ili kuwawezesha wananchi kutumia daraja hili usiku na mchana,” amesema Kasekenya.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo cha Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Dar es salaam, Mhandisi, Suzana Lucas amesema kwamba mvua zilizoanza kunyesha jijini Dar es salaam zimesababisha athari za miundombinu ya Barabara na madaraja yakiwemo lakini kazi ya kuiboresha miundombinu hiyo ili ipitike inaendelea na itakamilika katika muda mfupi ujao.
Ameyataja madaraja yalioothirika kuwa ni pamoja na daraja la Mtongani Kunduchi, daraja la Mpiji na daraja la Tegeta ambapo amemhakikishia naibu waziri kasekenya kuwa kazi zitafanyika usiku na mchna hadi zikamilike.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule ameshukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Raisi Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa walizofanya na kurudisha mawasiliano kwa haraka.
Ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari wakati wa mvua na kuwataka kusafisha mifereji na kuepuka shughuli za uharibifu wa mazingira katika mito inayopitisha maji ya mvua ili kulinda madaraja na barabara na hivyo kuepusha athari kwa wananchi.
Hata hivyo Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa angalizo la uwepo wa mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani (Ikijumuisha Visiwa vya Mafia), Njombe, Ruvuma, Morogoro, Lindi pamoja na Mtwara, huku wakitoa wito kwa mamlaka mbalimbali kuchukua tahadhari ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
Post a Comment