KAYA 72 YAHAMA HIFADHI YA NGORONGORO
Na Mwandishi wetu, Karatu Arusha.
Kundi lenye kaya 72 wananchi 515 na mifugo 2,206 limeagwa leo tarehe 18/01/2024 baada ya kujiandikisha na kuamua kuhama kwa hiyari kutoka katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera handeni Mkoani Tanga.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa zoezi hilo, meneja wa mradi wa kuhamisha wananchi waishio ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Fedes Mdala ameeleza kuwa baada ya kundi hili kuhama leo inafikisha jumla ya kaya 749 zenye watu 4,337 na mifugo 19,915 ambayo tayari zimehama ndani ya hifadhi kwenda maeneo yaliyopangwa na serikali pamoja na maeneo mengine ambayo wananchi wamechagua.
Kamishna wa Uhifadhi NCAA Richard Kiiza ameeleza kuwa kundi la awamu hii ndio kubwa zaidi kuondoka tangu kuanza utekelezaji wa zoezi hili na kuongeza kuwa kadri ujenzi wa Nyumba za makazi unavyoendelea Kijiji cha Msomera, kitwai na Saunyi idadi ya wananchi wanaojiandikisha kuhama kwa hiari imeendelea kuongezeka ambapo hadi sasa zaidi ya kaya 1,070 zimeshajiandikisha kuhama na zoezi la uhamasishaji na uelimishaji linaendelea.
Kamishna Kiiza ameongeza kuwa zoezi la ujenzi wa Nyumba 5,000 katika Kijiji cha Msomera, Saunyi na Kitwai linaendeela chini ya SUMA JKT na tayari zaidi ya nyumba 360 zimeshakamilika na nyumba zingine zaidi ya 2,000 na nyumba nyingine ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Kiiza amewahimiza wananchi walioagwa leo kuendelea kuwa mabalozi wa kuwahimiza wananchi waliobaki kujiandikisha kuhama kwa hiari ili wanufaike na Maisha bora yaliyoandaliwa na Serikali nje ya Hifadhi.
Akiwaaga wananchi hao Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Kanali Wilson Sakulo ameeleza kuwa wananchi wanaohama kwa hiyari wanapewa stahiki zao zote za msingi ikiwepo nyumba yenye hati kwenye eneo la ukubwa wa ekari 2.5, shamba la kulima la ekari tano, huduma za maji, shule, afya, barabara, mabwawa, majosho, minada, umeme na huduma za mawasiliano na kupata uhuru wa kufanya shughuli za kilimo na kuishi Maisha huru tofauti na hifadhini.
Kanali Sakulo ameelekeza uongozi wa NCAA kuendelea kutoa elimu, uhamasishaji na uandikishaji kwa wananchi walio tayari kuhama kwa hiari na kuhakikisha kuwa kila mwananchi aliyejiandikisha kuhama anahamishwa kwa wakati, kupata stahiki zake zote na kuhakikisha wananchi wanaohama hawarudi tena maeneo ambayo wameshahama kwa kuwa Serikali yetu imeshawajengea mazingira wezeshi yenye huduma zote muhimu za kijamii.
Mmoja ya wananchi aliyehama Petro Tengesi amemshukuru Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake kwa wananchi wa Ngorongoro na kuendelea kuwajengea mazingira bora nje ya hifadhi ikiwemo ulipwaji wa stahiki zao za kuhama, kusafirishiwa mizigo yao pamoja naa kuboreshewa huduma za kijamii nje ya hifadhi.
Post a Comment