Ads

SERIKALI KUMALIZA UTATA HIFADHI YA NGORONGORO

Na Francisco Peter

MSEMAJI Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO, Mobhare Matinyi amesema kuwa serikali inafanya tathmini ya kuwalipa kila Mwananchi mwenye mali anayomiliki katika hifadhi Ngorongoro na baada ya kuwalipa kwa kila kaya ikiwa ni pamoja na kupewa kiasi cha fedha cha Milioni 10, huku mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro itamhamisha kwa gharama zake bila kulipishwa muhusika yeye,mali zake ikiwemo mifugo pamoja na familia yake kwenda kwenye makazi mapya Msomera Mkoani Tanga.


Amesema hayo leo Desemba 3, 2023 katika mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo Cha Utalii kilichopo jijini Dar es Salaam.

"'Awamu ya kwanza ilianza sasa tupo kwenye utekelezaji awamu ya pili ambayo imeanza Julai 2023 na inatarajiwa kwenda mpaka Machi, 2024 huku lengo kubwa la serikali ni kujenga nyumba 5 ,000 katika eneo linalojumuisha Kitwai, Sauni na Msomera kwa ajili ya wakaazi wa Ngorongoro wanaohamia kwa hiyari eneo la Msomera." Amesema Matinyi.

Matinyi amesema kuwa kila mwananchi anajengewa nyumba yenye vyumba vitatu anapewa fursa ya kuunganishiwa umeme na TANESCO kwa gharama ya 27,000, huku Wizara ya Maji inachimba visima ambavyo vitakuwa na sehemu za kusambazia maji ili wananchi waweze kupata maji.

Amesema kuwa mbali na Tume inayoshughulika na masuala ya ardhi kufanya kazi ya kupima viwanja na viwanja hivyo kujengwa nyumba za kisasa pia kuna kazi ya kujenga barabara na kuweka mifumo ya umeme.

"Kuna Wizara zilikwenda Msomera zikaunda timu ya pamoja ili kufanya oparesheni hii ifanikiwe zipo Wizara kumi ambazo ni Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Maliasili na Utalii,Nishati,

Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Kilimo, Maji, Mifugo na Uvuvi, Maendeleo ya Jamii Watoto Jinsia wanawake na Makundi Maalumu Mambo ya Ndani, Katiba na Sheria.

Aidha Matinyi amesema kuwa Wizara ya kilimo imesema mbali na kuwatengea mashamba wameanzisha mashamba darasa kwa wakazi hao ili wananchi hawa waweze kulima mbali na shughuli walizokuwa wamezizoea awali za ufugaji.

Akifafanua kuhusu shughuli za kiuchumi amesema kuwa zinakwenda kuongezwa ili maisha ya wananchi hao yawe mazuri.

"Familia ambazo zimehamia pale kwa fedha zilizolipwa wameweza kujiendeleza na kujiendeleza kiuchumi huku baadhi yao wameanzisha shughuli za biashara na kuweza kukuza uchumi wao ambazo hapo awali hazikuwezekana walipokuwa wakiishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro ,wengine hivi sasa wanamiliki vyombo vya usafiri (Bodaboda) na wanafanya shughuli za kilimo.

Aidha shughuli za kiuchumi zinazidi kuongezwa ili maisha ya hawa wananchi yawe mazuri.

"Wizara ya Mifugo imekwenda kujenga mnada wa kisasa ili wananchi wapate shughuli za kiuchumi na imeongeza vituo vya kukusanyia maziwa, kwani wafugaji ukiacha uuzaji wa nyama kwenye mnada huwa wanauza maziwa kwa hiyo kutakuwa na vituo kwa ajili ya wananchi kupeleka maziwa na kupata pesa.

Wakati huohuo Msemaji Mkuu wa Serikali Matinyi ametoa wito kwa Asasi za Kiraia pamoja na vyombo vya nje ya nchi kuja nchini na kwenda Ngorongoro walikokua wakiishi wananchi kwenda kuangalia makazi mapya wanayoishi hivi sasa ili wasitoe taarifa potofu kwa nchi kwa sababu Serikali haiko tayari kuona wananchi wake wanaishi katika mazingira hatarishi na wanyama wakali ambao wamekuwa wakiwasababishia maafa ikiwemo vifo.

No comments