Ads

BENKI YA MAENDELEO YA TIB YAFANYA MAKUBWA

Na Francisco Peter

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema Benki ya maendeleo ya TIB mwanzo ikijulikana kama,’’Benki ya uwekezaji Tanzania’’ imefanya kazi kubwa katika uendelezaji wa miradi ya maendeleo nchini ikiwemo mkoa wa Dar es Salaam.

Chalamila aliyasema hayo jana alipokuwa mgeni rasmi katika mkutano mkuu wa majadiliano baina ya benki hiyo na wadau wa maendeleo wakiwemo wafanyabiashara, wawekezaji na taasisi za uma uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere (JNICC).

“Pasipo uwepo wa uwekezaji mkubwa unaofanywa na T.I.B huenda baadhi ya miradi mikubwa isingeendelea hapa nchini, chukulia kwanza umri wake kuanzia mwaka 1970 hadi leo imepitia mabonde na milima hata Dada yangu Kaimu Mkurugenzi mtendaji alikabidhiwa benki ikiwa dhaifu kwa namna nyingine lakini kwa maelezo ya leo (jana) kazi kubwa imefanyika na nichomekee ikimpendeza Dk Samia Suluhu Hassan Rais wa Tanzania amuidhinishe kuwa Mkurugenzi ili atimize wajibu wake bila woga” alisema

Sanjari na pongezi hizo, Chalamila alisema mkoa wake kupitia wananchi wake wamenufaika kwakukopeshwa zaidi ya Sh 110 bilioni ambazo zimeleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi mkoani humo.

Aidha Chalamila aliongeza kwamba kama siyo kazi nzuri inayofanywa na T.I.B yawezekana leo hii hata nishati ya umeme ambayo kwa asilimia 65 hutegemea gesi usingefanikiwa kwakuwa benki hiyo ndiyo inayowakopesha wawekezaji katika nishati ya gesi na asilimia 35 za umeme wa maji pia benki hiyo ina mchango mkubwa kwa shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambapo nao ni sehemu ya wadau wa T.I.B

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake kwa robo waka 2023 iliyoishia Septemba 30 ,2023, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa T.I.B, Liliani Mmbassy alisema wanasimamia miradi ya sekta binafsi kwa 93% na ya serikali ikiwa ni 7% ambapo miradi yao ni kuanzia miaka 5 hadi 20 huku ikijikita zaidi katika wawekezaji wa ndani.

Hadi kufikia Septemba 30, 2023 benki hiyo imewekeza Sh 253 bilioni kwa mikoa 23, wilaya 76 zikinufaika katika miradi mbalimbali ikiwemo maji, umeme na kilimo.

“Tumewekeza katika miradi mbalimbali kama kilimo 34%, madini20%, utalii 15% na sekta nyinginezo kama nishati, ujenzi na kwingineko tupo, ni mengi tumefanya tuiombe serikali izidi kutuunga mkono” alisema Lilian.

Benki hiyo iliundwa 1970 kwa malengo mahususi ya kutoa mikopo kwa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali lakini baadaye sekta binafsi pia zikahusika kwa maendeleo ya nchi.Mengineyo ni ushauri wa kitaalamu na ufundi, kusimamia mifuko mbalimbali ili itekeleze miradi ya maendeo.

No comments