Ads

WANANCHI WA IGULA WAPATA MAJI YA RUWASA YATUMIA ZAIDI YA MILIONI 560 KUTEKELEZA MRADI MKUBWA WA MAJI

 

Tenki lenye uwezo wa kuchukua lita 150,000 za maji lililojengwa na wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kupitia mradi wa maji wa kijiji cha Igula wilayani Wanging,ombe mkoani Njombe ambalo linahudumia  wakazi wa kijiji hicho.
Msimamiz wa ujenzi wa mradi wa maji Igula wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe Mhandisi Joseph Peter akitoa maelezo juu ya miundimbinu ya  ujenzi wa mradi huo kwa baadhi ya viongozi wa serikali cha Igula,kulia Mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Wanging'ombe(WANGIWASA) Mussa Masasi na wa tatu kushoto Kaimu Meneja wa Ruwasa wilayani Wanging'ombe Msafiri Tematema.
Baadhi ya waandisi wa Ruwasa wilaya ya Wanging,ombe na kutoka  Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira wilaya ya Wanging'ombe(WANGIWASA)wakikagua baadhi ya miundombinu katika mradi wa maji wa kijiji cha Igula uliotekelezwa na Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilayani humo kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uvico-19.
Wataalam kutoka wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(RUWASA) na mamlaka ya  maji safi na usafi wa mazingira Wilaya ya Wanging'ombe(WANGIWASA) wakikagua kituo cha kuchotea maji katika kijiji cha Igula wilayani humo ambacho ni miongoni mwa vituo vilivyojengwa kwa ajili ya kutoa huduma ya maji kwa wananchi


Na Muhidin Amri,

Wanging’ombe

SERIKALI imetumia Sh.milioni  560,788,295  kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uvico-19,kutekeleza  mradi mkubwa ya maji katika kijiji  vya Igula Halmashauri ya wilaya Wanging’ombe mkoani Njombe.

Fedha hizo zimewezesha kumaliza  kabisa kero ya maji safi na salama iliyokuwa inawakabili wakazi 1,780 wa vitongoji vya Azimio,Kidegenge,Kiginga, na Mlowa ambao kwa sasa wanapata huduma ya maji safi na salama kwa masaa 24.


Hayo yamesemwa na kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Wanging’ombe Msafiri Tematema,wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo kwa Waandishi wa habari walioko kwenye ziara ya kutembelea miradi ya maji  inayotekelezwa na wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) katika mikoa nyanda za juu kusini.


Tematema alisema, chanzo kikuu cha mradi huo ni kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha maji lita 10,000 kwa saa ambacho kimefungwa pampu yenye uwezo wa kuvuta maji lita 8,000 kwa saa.


Alisema,kazi ya ujenzi wa mradi imekamilika kwa asilimia 100 na  sasa wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama katika maeneo yao,hivyo kuondokana na adha kubwa ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji kwenye vyanzo na visima vya asili.


Alieleza kuwa,serikali kupiti wakala wa maji safi na usafi wa mazingira(Ruwasa) wilaya ya Wanging’ombe na mkoa wa Njombe,imeamua kujenga mradi huo kutokana  na upungufu mkubwa wa maji katika kijiji hicho ambacho kinahudumiwa na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mzingira Wanging’ombe(WANGIWASA).


Aidha alisema, Ruwasa wilaya ya Wanging’ombe imekamilisha mradi mwingine wa maji katika kijiji cha Samaria na kuboresha huduma ya  upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi 1,873 wa kijiji hicho.

Alisema,mradi huo umetekelezwa kwa njia ya Force Akaunti kwa gharama ya Sh.milioni 380 na zimetumika kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na umekamilika kwa asilimia 100.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Wanging’ombe(WANGIWASA) Mussa Masasi alisema,mamlaka hiyo inatoa huduma ya maji kwa vijiji 54  vilivyopo katika wilaya ya Wanging’ombe kikiwemo kijiji cha Igula.


Alisema,mradi huo umetokana na maombi kutoka kwa uongozi wa serikali ya kijiji cha Igula  kutaka kuchimbiwa kisima ili kukabiliana na kero ya huduma ya maji,hata hivyo mamlaka haikuwa na fedha na walipeleka ombi hilo kwa Ruwasa ili iweze kuwasaidia.

Masasi,ameishukuru Ruwasa kutoa  kiasi cha Sh.milioni 560,788,295 ambazo zimefanikisha kukamilika kwa mradi huo  na sasa wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama katika maeneo yao.


Alisema baada ya kukamilika kwa mradi huo,kazi kubwa inayofanyika  kwa sasa ni mamlaka kuongeza wateja wengi zaidi ili kupata mapato ambayo yatawezesha kujiendesha,kuboresha huduma na kupanua mtandao kwa lengo la kuwapunguzia  wananchi muda wa kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji.

Pia alisema kuwa, kabla ya kujengwa kwa mradi huo mapato ya mamlaka  hayakuzidi shilingi milioni 1 kwa mwezi,lakini ni matumaini yake kupitia mradi huo mpya mapato yataongezeka hadi kufika milioni 7 kwa mwezi.

Amewataka wananchi,kuhakikisha wanalinda miundombinu na  kutunza miradi inayojengwa,kutumia maji kwa uangalifu  na kulipia gharama za maji ili kuijengea uwezo mamlaka hiyo iweze kujiendesha bila kutegemea ruzuku na msaada kutoka serikali kuu.

Mkazi wa kijiji cha Igula Aisha Athuman alisema, shida ya maji katika kijiji hicho ilikuwa kubwa ambapo walilazimika kwenda hadi kijiji jirani cha Ilembula kufuata huduma maji kwa matumizi ya kila siku.

Alisema,ukosefu wa maji safi na salama ulipelekea hata wanafunzi kushindwa kuhudhuria vipindi hasa wakati wa asubuhi  kwa kuwa walilazimika kwenda  mtoni kutafuta maji kwa ajili ya usafi wa mazingira na matumizi mengine kabla ya kuingia darasani na hivyo kuathirika sana kitaaluma.

No comments