Ads

RAIS DKT. SAMIA AFANYA MAKUBWA MRADI WA KUFUA UMEME JNHPP RUFIJI

Na Francisco Peter.

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) uliopo Rufiji mkoani Pwani, umeonesha kuwa Watanzania wanaweza mambo makubwa.

Dkt. Samia amesayema hayo leo Desemba 22, 2022 mkoani Pwani akizungumza katika hafla ya ujazaji maji katika Bwawa hilo, mradi ambao ukikamilika utazalisha Megawati 2115 za umeme.

“Mradi huu unatoa ujumbe Duniani kwamba Tanzania inaweza kutekeleza mambo makubwa ya kuweza kubadilisha hata taswira yake na ya ulimwengu kwani Bwawa hili linaonekana kutoka anga za juu kabisa na kuweza kuwa na alama katika ramani mpya ya Dunia,” amesema Rais Dkt. Samia.

Rais Dkt. Samia amesema mradi huu utaipatia Tanzania umeme wa uhakika kwa ajili ya maendeleo endelevu na kutimiza ndoto iliyokuwepo tangy zamani kutokana na fikra za viongozi waliopita mwanzilishi akiwa ni Hayati Mwal. Julius Nyerere Rais wa Awamu ya Kwanza.

Amesema kwamba mradi huo ulianza utekelezwaji wa ujenzi wake mwaka 2018 katika Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Hayati Rais Dkt. John Magufuli.

Hata hivyo anapata faraja kwamba wakati anakabidhiwa jukumu la kuongoza nchi, mradi huo ulikuwa kwenye asilimia 37 lakini hadi sasa umefikia asilimia 78.78.

“Na leo kwa dhati kabisa namshukuru Mungu wangu na napata faraja kuona mradi huu uko kwenye asilimia 78.78 na nataka nitoe ahadi kwenu ndugu Watanzania kwamba nitausimamia mradi huu hadi ukamilike kama ulivyopangwa,” amesema Rais Dkt. Samia.

Ameongeza kuwa Bwawa hilo litaweza kuweka akiba kubwa ya maji na kuzalisha umeme hata pale mvua inapokuwa imepungua, vile vile ameeleza kwamba litasaidia kudhibiti mafuriko ya mara kwa mara ya Mto Rufiji na kuwezesha kilomo cha umwagiliaji pamoja na kukuza utalii.

Waziri wa Nishati January Makamba amesema ni mradi mkubwa, wa gharama kubwa na wajasho la Watanzania.

Amesema hatua ya kuanza kujazwa maji inatakiwa kushuhudiwa na Rais, Viongozi mbalimbali na wananchi kwani matukio kama hilo kwa miradi mikubwa ni jambo la kawaida.

No comments