TFNC YAITAKA JAMII KUHIFADHI CHAKULA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA HALI YA HEWA.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) imeitaka jamii kujipanga kula Chakula mchanganyiko kinachoweza kupatikana katika msimu mvua katika kipindi cha mwezi wa Novemba, 2022 hadi April, 2023 ili kukidhi mahitaji ya lishe.
Hatua hiyo imekuja baada Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) October 26, 2022 kutoa utabiri wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka katika kipindi cha mwezi wa Novemba 2022 hadi April 2023.
Utabiri huo umeonesha nusu ya kwanza wa msimu kuanzia Novemba, 2022 hadi Januari, 2023 kutakuwa na vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa kujitokeza katika maeneo inayojumuisha mikoa ya Tabara, Mbeya, Njombe, Iringa, Ruvuma, Morogoro Kusini, Kigoma Kusini, Ruvuma, Katavi ambayo inazalisha chakula kwa wingi nhini Tanzania.
Akizungumza na mwandishi wetu jijini Dar es Salaam Afisa Lishe Mtafiti, Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe Bw. Walbert Mgeni, amesema kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanaathiri sekta ya lishe kwa sababu yanaleta upungufu wa mvua na kusababisha kupungua kwa kasi ya kuzalisha mazao mashambani.
Bw. Mgeni amesema kuwa jamii inapaswa kula mlo mchanganyiko unaopatikana kutoka makundi mbalimbali ya chakula jambo ambalo litasaidia lishe kuimarika.
"Sekta ya kilimo inatakiwa kuendelea kutoa ushauri kwa wakulima ili waweze kulima mazao yanaoendana na mabadiliko ya hali ya hewa ili kuepuka ukosefu wa chakula cha kutosha unaweza kuathiri lishe katika jamii" amesema Bw. Mgeni.
Amesema tayari baadhi ya vyakula vimeanza kupanda bei na kusababisha familia zenye kipato kidogo kushindwa kumudu gharama.
Amefafanua kuwa jamii inapaswa kuifadhi chakula ili kuhakikisha lishe bora inapatikana katika familia.
Afisa huyo wa Lishe amewataka wakulima kulima mazao yanayostahimili ukame ikiwemo mtama, mihogo, mahindi pamoja na kuepuka kulima mazao yanayohitaji mvua nyingi.
"Kuna mabadiliko ya hali ya hewa, jamii inatakiwa kuzingatia mlo kamili pamoja kulima mazao ambayo yanaendana na mabadiliko ya hali ya hewa" amesema Bw. Mgeni.
Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania inaendea kutoa wito kwa jamii kula vyakula mchanganyiko kutoka makundi mbalimbali ikiwemo vyakula vya nafaka (ndizi mbichi, mahindi, mtama, ulezi, ngano), vyakula vya asili ya wanyama na jamii ya mikunde, mboga mboga, matunda pamoja na sukari, mafuta na asali.
Post a Comment