TAKUKURU TEMEKE YAONGEZA KASI UFATILIAJI WA MIRADI YA KIMAENDELEO.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bw.
Holle Makungu akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu taarifa utekelezaji wa
majukumu kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia January hadi March 2022.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES
SALAAM.
Taasisi ya Kuzui na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imejipanga kuendelea kuongeza
kasi ya ufatiliaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo ili kuziba mianya ya
rushwa hasa katika sekta ya ujenzi ambapo serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi.
Akizumgumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu utekelezaji wa majukumu
yake kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia January hadi March 2022, Mkuu
wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke, Bw. Holle Makungu amesema kuwa wamefanikiwa
kufatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara zenye thamani
ya zaidi ya bilioni moja.
Bw. Makungu amesema kuwa
wamefatilia utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Mvomero, Ngomano na Keko
Machungwa zenye gharama ya Tsh. 447,052, 367 ambazo zipo katika Jimbo la Temete.
Amesema wamefatilia ujenzi
wa barabara ya Jeshini – Kizuiani yenye gharama ya Tsh. 165, 704, 740, barabara
ya Machinjio za Jimbo la Mbagala zenye gharama ya Tsh. 307, 588, 300.
Barabara za Tungi,
Mjimwema na Upendoyeye zenye gharama ya Tsh. 467, 752, 466. 40 pamoja na ujenzi
wa Bweni katika Shule ya Msingi ya Chekenimwasonga yenye gharama ya Tsh 80,000,
000.
”Baadhi ya miradi
iliyofanyiwa ufatiliaji imebainika kuwa na mapungufu ya ucheleweshaji wa utekelezaji,
ucheleweshaji wa malipo ya mkandarasi, hivyo tumewashauri watendaji kutekeleza
na kukamilisha miradi hiyo kwa wakati ili kufikia lengo lililokusudiwa” amesema
Bw. Makungu.
Bw. Makunga amesema kuna
jumla ya mashauri 19 yanaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Mkoa wa Temeke,
huku akibainisha kuwa wamepokea malalamiko 75 katika ya hayo 49 yanahusu rushwa
na 26 malalamiko yasiyohusu rushwa.
Amebainisha kuwa
malalamiko 49 yaliyohusu rushwa uchunguzi wake umekamilika, na majalada 10
yamefungwa kwa kukosa ushaidi huku mjalada 30 uchunguzi wake bado unaendelea.
“Ili kuhakikisha elimu ya mapambano
dhidi ya rushwa inawafikia watu wengi, tumeendelea kuelimisha jamii kupitia
njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari, semina, mikutano ya hadhara pamoja
na kushiriki maonesho mbalimbali” amesema Bw. Makungu.
Ametoa wito kwa wananchi kila mmoja kuwajibika kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kuunganisha nguvu kwa pamoja, kuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa ya vitendo vya rushwa.
Post a Comment