MKURUGENZI TMA DKT. KIJAZI AELEZA MAKUBWA MABORESHA UTENDAJI WA UTABIRI WA HALI YA HEWA.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imejipanga kuaendelea kutimiza jukumu la kuiwakilisha nchi katika masuala ya hali ya hewa kikanda na kimataifa na kutimiza makubaliano ambayo Tanzania imeridhia kimataifa katika masuala ya hali ya hewa ikiwemo kubadilishana data za hali ya hewa katika mtandao wa Dunia (Global Telecomunication System-GTS).
Imebainika ili kufikia malengo tarajiwa TMA imeendelea kuwajengea uwezo wataalam kuelewa zaidi namna ya kukabiliana na mabadiliko hayo ya hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na kuwapeleka kupata elimu zaidi na tafiti mbalimbali za hali ya hewa.
Akifanya Mahojiani Maalam na mwandishi wetu hivi karibuni jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Agnes Kijazi, amesema kuwa serikali inaendelea kuwezesha uboreshaji na upanuzi wa mtandao wa vituo vya hali ya hewa nchini kila mwaka pamoja na upanuzi ambao utasaidia Mamlaka kutoa taarifa za hali ya hewa katika maeneo madogo madogo kwa usahihi zaidi.
“Tunaendelea kuboresha Chuo cha Hali ya Hewa cha Taifa kilichopo Kigoma, kwa kuendelea kuzalisha wataalamu wa Hali ya Hewa kwa ngazi za Cheti na Diploma, pia tutashirikiana na vyuo vya elimu ya juu nchini katika kuongeza ujuzi wa wataalamu wetu hususan Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho kinatoa Shahada ya sayansi ya hali ya hewa (BSc in Meteorology) na Shahada ya Uzamili katika masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi (MSc. in Climate Change)’’ amesema Dkt. Kijazi.
SWALI.
Mwandishi wa Habari : Kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni tumekuwa mashuhuda wa kazi kubwa inayofanywa na TMA kwa uhakika na wakati, nini siri ya hali hii?
MAJIBU. Dkt. Agnes Kijazi : Hali hii imechangiwa na uboreshaji katika maeneo mengi ikiwemo Uboreshaji wa vifaa vya hali ya hewa; awali ya yote, naishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa awamu ya sita kwa kuendelea kuboresha na kuongeza miundombinu ya uangazi na uchambuzi wa taarifa za hali ya hewa ikiwemo vifaa vya kisasa vya hali ya hewa ikiwa pamoja na Radar za hali ya hewa, Komputa zenye uwezo mkubwa (Cluster Computer) na vituo vya uangazi vinavyojiendesha vyenyewe-Automatic Weather Stations ambavyo vimesaidia sana kuboresha huduma za hali ya hewa hapa nchini.
Pia Wataalamu Kuongezewa ujuzi; Napenda kuishukuru Serikali na Wafadhili ambao wameendelea kugharimia mafunzo ya wataalamu wa wa hali ya hewa na hivyo kuiwezesha Mamlaka kuwa na wataalamu wenye ujuzi na uzoefu wa kutosha kutafsiri mifumo ya hali ya hewa. Uwepo wa wataalamu umeiwezesha Mamlaka kuongezeka viwango vya usahihi wa utabiri wa hali ya hewa na hivyo kufikia matarajio ya wadau wetu.
Wataalamu wa TMA kubuni mifumo ya TEHAMA: Mamlaka ina mifumo mitatu (3) ambayo imebuniwa na wataalamu wake inayohusu uangazi, mawasiliano ya data na uchambuzi (Digital Meteorological Observatory-DMO, Meteorological Aviation Information System-MAIS na Meteorological Marine Information System-MMIS). Mifumo hii imepunguza gharama za uendeshaji na hivyo kuboresha huduma zinazotolewa na Mamlaka katika sekta ya Usafiri wa Anga, watumiaji wa bahari na maziwa pamoja na ubadilishanaji wa taarifa za hali ya hewa.
Kuanzishwa kwa Shahada ya Hali ya Hewa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam: Serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kusomesha wataalamu wa hali ya hewa nje ya nchi hivyo kuanzishwa kwa shahada ya hali ya hewa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam imepunguza gharama za mafunzo na kuongeza wataalamu katika Mamlaka. Hali ambayo imesaidia kuboresha huduma.
SWALI.
Mwandishi wa Habari
: TMA ni moja ya taasisi chache
zinazoshughulika na masuala ya utabiri wa hali ya hewa Afrika, ambazo
zinazoongozwa na Mwanamke, lakini ni pekee kati ya hizo iliyofanikiwa kupata
nafasi kwenye ngazi za juu za uongozi katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani,
mnalizungumziaje hili?
MAJIBU. Dkt. Agnes Kijazi : Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi ambazo tumepata kuiwakilisha Tanzania Kimataifa katika masuala ya hali ya hewa, hili pia ni jukumu mojawapo la Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuiwakilisha Tanzania kimataifa katika masuala ya hali ya hewa.
Kilichonisaidia kupata nafasi niliyo nayo sasa ya Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ni pamoja na Kuungwa mkono na Serikali : Ili uweze kugombea ni lazima upitishwe na Serikali ya Nchi yako. Napenda kuishukuru Serikali kwa sababu ilipendekeza jina langu kugombea nafasi ya Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO.
Kukubalika kwa Tanzania Kimataifa: Ili kuchaguliwa lazima nchi yako ikubalike kimataifa.Namshukuru Mungu kwa sababu Tanzania inaheshimika na kukubalika katika nyanja za kimataifa, hali iliyosaidia mimi kuchaguliwa katika nafasi hiyo.
Sifa nilizonazo katika sekta ya hali ya hewa : Ili uweze kupigiwa kura na nchi Wanachama wa WMO lazima uwe na sifa zinazokubalika. Namshukuru Mungu kwa sababu pamoja na elimu niliyo nayo nimeweza kusimamia vyema taasisi yetu ya hali ya hewa hapa nchini pamoja na kutekeleza vyema majukumu yote ambayo nimepewa kimataifa katika nafasi yangu ya Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani. Sifa hizo na ujuzi nilio nao umesaidia kupigiwa kura na kupata nafasi hii.
Ushirikiano ndani ya TMA : Hali ya utulivu na ushirikiano katika Taasisi ambayo mgombea anaiongoza ni sifa mojawapo inayomwezesha kuchaguliwa. Namshukuru Mungu kwa ushirikiano na ‘Team Work’ iliyopo ndani ya TMA ambavyo vimewezesha wataalamu wa TMA walioko katika vikosikazi mbalimbali vya WMO kufanya vizuri. Aidha, TMA imefanikiwa kuongeza viwango vya usahihi wa utabiri wa hali ya hewa na kupata fursa ya kuzisaidia nchi nyingine, hali ambayo imesaidia mimi kuchaguliwa katika nafasi hiyo.
SWALI.
Mwandishi wa Habari
: Malengo ya TMA kiufanisi ndani ya
miaka kadhaa ijayo hususan chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ni
yepi?
MAJIBU. Dkt. Agnes Kijazi : Kitaifa ni kuendelea kutekeleza majukumu yote ambayo TMA imekasimiwa kisheria ikiwemo kutoa, kudhibiti na kuratibu huduma za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Majukumu haya ni
pamoja na Kuendelea kutoa huduma bora
za hali ya hewa na kupanua wigo wa ukusanyaji wa taarifa za hali ya hewa.
Upanuzi wa mtandao wa vituo vya hali ya hewa utakaosaidia Mamlaka kutoa taarifa
za hali ya hewa katika maeneo madogo madogo kwa usahihi zaidi.
Kuendeleza ushirikiano wa karibu na vyombo mbalimbali vya habari ikiwa ni pamoja na kuandaa warsha mbalimbali zenye lengo la kuelimisha kuhusu sayansi ya hali ya hewa na hivyo kusaidia katika matumizi ya lugha nyepesi, sahihi na kuwafikia wananchi kwa wakati.
Mfano TMA hufanya warsha za wadau mbalimbali (Wanahabari, wakulima, wavuvi, nishati, afya, madini, uchukuzi n.k) mara kwa mara hususan kabla ya kutolewa rasmi kwa taarifa ya mwelekeo wa mvua kwa msimu husika, ambapo Mamlaka inashirikiana na vyombo vya habari takribani 90 zikiwemo redio jamii (local radio) katika kusambaza utabiri wa kila siku, msimu na tahadhari za hali mbaya ya hewa.
Kuongeza wigo wa mifumo ya usambazaji ikiwemo Mitandao ya kijamii; Kuboresha namna ya usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kwa kupitia ofisi zetu za kanda na mikoa, mitandao ya kijamii.
Kushirikiana na ofisi za serikali za mitaa ambao wako karibu zaidi na wananchi, kwa mfano; taarifa zinazohusu kilimo tutazifikisha moja kwa moja kwa maafisa ugani ili wazitumie katika shughuli za kilimo.
Kuweka juhudi ili kuendelea kushikilia cheti cha ubora (ISO 9001:2015) cha huduma za hali ya hewa, kuendelea kuwajengea uwezo watumiaji wa taarifa na wadau wengine wa huduma za hali ya hewa katika kuzielewa na kuzitumia ipasavyo taarifa za hali ya hewa.
Kuendelea kuboresha Chuo cha Hali ya Hewa cha Taifa kilichopo Kigoma, kwa kuendelea kuzalisha wataalamu wa Hali ya Hewa kwa ngazi za Cheti na Diploma.
Aidha, tutaendelea kushirikiana na vyuo vya elimu ya juu nchini katika kuongeza ujuzi wa wataalamu wetu hususan Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho kinatoa Shahada ya sayansi ya hali ya hewa (BSc in Meteorology) na Shahada ya Uzamili katika masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi (MSc. in Climate Change), hivyo kuongeza watalamu wa Hali ya Hewa kwenye soko la ajira.
Kuendelea kutekeleza program ya mafunzo ya Mamlaka (Training Program) ili kuwaongeza wataalamu wa hali ya hewa ujuzi, kuboresha maslahi ya wataalamu wa hali ya hewa ili kuwaongezea ari ya kufanya kazi, kuboresha mazingira ya kazi ikiwemo ofisi za TMA, kuboresha huduma za hali ya hewa zinazotumika kibiashara ili kuongeza mapato ya Taasisi.
Kimataifa: TMA itaendelea kutimiza jukumu la kuiwakilisha nchi katika masuala ya hali ya hewa kikanda na kimataifa na kutimiza makubaliano ambayo Tanzania imeridhia kimataifa katika masuala ya hali ya hewa ikiwemo kubadilishana data za hali ya hewa katika mtandao wa Dunia (Global Telecomunication System-GTS).
SWALI.
Mwandishi wa Habari
: Changamoto zipi bado ni kikwazo kwa
ufanisi wa taasisi na mmefanya jitihada gani kuzitatua?
MAJIBU. Dkt. Agnes Kijazi : Upungufu wa vituo vya ukusanyaji wa taarifa: Ili kuendelea kutoa huduma bora za hali ya hewa, Mamlaka bado ina uhitaji wa kupanua wigo wa ukusanyaji wa taarifa za hali ya hewa.
Jitihada: Serikali yetu hutenga bajeti na inaendelea kuwezesha uboreshaji na upanuzi wa mtandao wa vituo vya hali ya hewa nchini kila mwaka. Upanuzi huu utasaidia Mamlaka kutoa taarifa za hali ya hewa katika maeneo madogo madogo kwa usahihi zaidi.
Uelewa mdogo wa taarifa na huduma zinazotolewa na Mamlaka kwa wadau. Jitihada: Kuendelea kutoa elimu kwa wadau ili waweze kuzielewa taarifa na kuzitumia ipasavyo katika shughuli zao mbalimbali za maendeleo.
Mabadiliko ya hali ya hewa: Mabadiliko ya hali ya hewa Duniani yamekuwa yakiathiri mifumo ya hali ya hewa, wakati mwingine mabadiliko hayo hutokea katikati ya msimu wa mvua.
Jitihada: Mamlaka inaendelea kuwajengea uwezo wataalam ili kuelewa zaidi namna ya kukabiliana na mabadiliko hayo ya hali ya hewa. Ikiwa ni pamoja na kuwapeleka kupata elimu zaidi na tafiti mbalimbali za hali ya hewa.
Uelewa mdogo wa sheria Na. 2 ya 2019 iliyoianzisha Mamlaka ya Hali ya Hewa. Jitihada: Kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kwa kuandaa vipindi, makongamano na kila fursa inapojitokeza.
Post a Comment