TBS YATOA MAFUNZO YA UDHIBITI SUMUKUVU KWA WAZALISHAJI NA WASINDIKAJI WA MAZAO MKOA WA TANGA.
Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mhe. Hashim Mgandilwa amelipongeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa jitihada inazozifanya za kuendesha mafunzo kwa lengo la kuelimisha wajasiriamali na umma kwa ujumla juu viwango na ubora wa bidhaa hususani bidhaa za chakula.
Ametoa pongezi hizo leo tarehe 29/03/2022 wakati akifungua mafunzo kuhusu
udhibiti wa Sumukuvu kwa mazao ya mahindi, karanga, Viungo vya chakula pamoja
na bidhaa zake kwa wajasiriamali kutoka katika Jiji la Tanga.
Amesema Umuhimu wa chakula unasababisha suala la usalama kupewa kipaumbele
katika kulinda afya ya jamii na uchumi wa nchi na kuwa kigezo muhimu katika
biashara ya kitaifa na kimataifa.
"Chakula kisicho salama husababisha madhara ya kiafya na hata vifo kwa
walaji pamoja na kusababisha athari za kiuchumi. Hata hivyo, usalama wa chakula
unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchafuzi wa sumukuvu
ambayo husababisha madhara ya kiafya na hata kiuchumi". Amesema
Amewasihi wasindikaji na wazalishaji wa mazao kuzingatia mikakati ya
kukabiliana na changamoto ya sumukuvu ili vyakula vyetu viendelee kuwa salama
kwa muda wote.
Meneja wa Mafunzo na Utafiti Mwl.Hamisi Mwanasala amesema mafunzo hayo ni
mojawapo ya fursa muhimu ya kuelimisha jamii juu ya kukabiliana na sumukuvu ili
kulinda afya za wananchi na kuwezesha biashara ya chakula.
"Ili kuimarisha usalama wa chakula dhidi ya sumukuvu, TBS inatekeleza
mikakati mbalimbali, ikiwemo udhibiti wa sumukuvu kwenye chakula hususani mazao
ya mahindi, karanga na viungo vya chakula ambayo ndiyo yenye uwezekano mkubwa
wa kuchafuliwa na sumukuvu". Amesema Mwl.Mwanasala.
Amesema TBS inatoa elimu kwa wadau katika mnyororo wa thamani wa mazao ya chakula kwani jamii ikielimika itatoa mchango zaidi katika kukabiliana na sumukuvu.
Post a Comment