AGIZO LA WAZIRI JAFO KUHUSU TATHMINI ZA ATHARI KWA MAZINGIRA KUZINGATIA SHERIA NA TAKWIMU ZA HALI YA HEWA
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo akizungumza jambo
katika warsha ya wadau wa mazingira kuhusu umuhimu wa huduma za hali ya hewa,
iliyofanyika katika Ukumbi wa Maktaba, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tarehe
18/02/2022.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya
Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi akizungumza
jambo katika warsha ya wadau wa mazingira kuhusu umuhimu wa huduma za hali ya
hewa, iliyofanyika katika Ukumbi wa Maktaba, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
tarehe 18/02/2022.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo amewaagiza wadau wa mazingira kuzingatia
takwimu za hali ya hewa katika kuandaa tathmini za athari kwa mazingira nchini
ili kutekeleza matakwa ya sheria Na.2 ya mwaka 2019 ya Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania.
Mhe. Jafo ametoa maelekezo
hayo wakati akifungua rasmi warsha ya wadau wa mazingira kuhusu umuhimu wa
huduma za hali ya hewa, iliyofanyika katika Ukumbi wa Maktaba, Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, tarehe 18/02/2022.
“Nikiwa waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) nitahakikisha kabla ya kutoa
vyeti tathmini za athari kwa mazingira (EIA), jambo kubwa nitakaloliangalia ni
chanzo cha takwimu zilizoambatishwa, hivyo hakuna namna ya kukwepa, tutumie takwimu
sahihi za hali ya hewa kwa mustakhabali wa nchi yetu”. amesema Mhe.Jafo.
“Kila mradi unaotaka
kuwekezwa unatakiwa kufanyiwa tathimini za athari za mazingira (EIA), na
mchakato wa EIA ni lazima unahitaji takwimu za hali ya hewa, na ikitokea
umekosea takwimu utaleta shida”. amesema Mhe. Jafo.
Mhe. Jafo ameeleza
kuwa sheria Na.2 ya mwaka 2019 ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaipa
Mamlaka ya Hali ya Hewa jukumu la kutoa takwimu za hali ya hewa na kuzitaka
wizara, taasisi na wataalam elekezi wa mazingira (consultants) kuzingatia
umuhimu wa matumizi ya takwimu za hali ya hewa na endapo takwimu hizo
zitakosekana inatakiwa kupata ushauri wa kitaalamu kutoka TMA na kutokufanya
hivyo ni kuvunja sheria za nchi.
Mhe. Jafo amesema warsha
hiyo imetokana na mchakato wa kisheria ambapo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania lilipitisha sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania mwaka 2019 na
kanuni zake kusainiwa mwaka 2021, hivyo kupelekea taasisi tatu ambazo ni Baraza
la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA) na Chama cha Wataalam wa Mazingira Tanzania (TEEA) kuona umuhimu
wa kubadilishana mawazo ya namna ya kutekeleza sheria hiyo.
Mhe. Jafo amewataka TMA
kuandaa semina kwa maafisa mazingira waliopo katika halmashauri na mikoa yote
nchini ili wafahamu vyema masuala muhimu ya hali ya hewa kama ilivyoainishwa
katika sheria. Pia aliwataka (TMA) na kutoa mada kwenye vikao vya wakurugenzi
wa jiji na halmashauri, ili kuwajengea uelewa wa sheria hiyo Na. 2 ya mwaka
2019.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA na
Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes
Kijazi ameeleza kuwa warsha hii ni fursa
muhimu ya kuboresha huduma katika sekta ya mazingira kwa kuzingatia matumizi
sahihi ya huduma za hali ya hewa zinazotolewa na TMA na matakwa ya kisheria
pamoja na kuimarisha uelewa kuhusiana na changamoto za mabadiliko ya hali ya
hewa na tabia nchi.
Dkt. Kijazi amewajulisha
washiriki wa warsha hiyo kwamba huduma za hali ya hewa zinazotolewa nchini
zimeongezeka viwango vya usahihi hivyo zinafaa kutumika katika sekta zote za
maendeleo.
Mwakilishi wa Mkurugenzi
Mkuu wa NEMC, Bi Lilian Lukambuzi amesema NEMC na TMA wameingia makubaliano
yenye lengo la kufanya tafiti za pamoja kuhusu masuala ya ya hali ya hewa na
mazingira na kufuatilia miradi ya
kimkakati ili kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu.
Mwakilishi wa TEEA Bi.
Rukia Ismail alifafanua kuwa warsha hiyo itawasaidia katika kuimarisha ufanisi wa kuandaa
thathmini za athari kwa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi kwa kutatua
changamoto mbalimbali zinazowakabili wadau wa mazingira katika utekelezaji wa
majukumu yao ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa takwimu za muda mrefu za hali ya
hewa.
Warsha ya wadau wa
mazingira kuhusu umuhimu wa huduma za hali ya hewa imeandaliwa kwa ushirikiano
wa TMA, NEMC na TEEA ikiwa na lengo la kujenga uelewa kuhusu taarifa za hali ya
hewa na umuhimu wa kuzingatia mipango ya utekelezaji wa mipango hiyo.
Post a Comment