WAZIRI GWAJIMA AWAKABA WANAUME DHIDI YA UKEKETAJI
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akisalimiana na watoto katika Kituo cha City of Hope kwenye Shule ya Kumbukumbu ya Dkt. John Chacha iliyoko Tarime, Mkoani Mara. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dorothy Gwajima akizungumza na wanafunzi na watumishi katika Shule ya Kumbukumbu ya Dkt. John Chacha iliyoko Tarime, Mkoani Mara.
Mwandishi Wetu, Tarime
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema wakati umefika kwa jamii kuachana na vingizio vinavyosababisha kuendelea kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto na badala yake kusimamia misingi ya upatikanaji wa haki.
Waziri Dkt. Gwajima amesema hayo Wilayani Tarime Mkoa wa Mara alipotembelea kituo Nyumba Salama cha Masanga kinachotumika kuwalea watoto waliokumbwa na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia au walio katika hatari ya kukumbwa na vitendo hivyo.
“Jamii lazima ishiriki kikamilifu kufuatilia matatizo yanayowakumba wanajamii husika na kama wanashindwa kufanya hivyo wanakuwa wanahusika kwa namna moja au nyingine na vitendo hivyo” alisema Dkt. Gwajima
Aliongeza kuwa katika baadhi ya maeneo nchini watoto wanafanyiwa vitendo vya kikatili na kukoseshwa haki ya elimu ilhali watumishi wanaopaswa kuingilia kati suala hilo wanabaki kimya na kuongeza kuwa baadhi ya watendaji katika ngazi mbalimbali wanabweteka na kulipwa mshahara bila kuufanyia kazi.
Wakati huo huo Waziri Dkt. Gwajima ametuma salamu kwa watendaji wa moja ya Mtaa na Kata Mkoani Mwanza ambao aliishi mtoto mmoja aliyekoseshwa haki ya kwenda shule ili abaki nyumbani akimuuguza Bibi yake wakati watendaji hao wapo katika eneo hilo.
“Mwanza mwambieni, Mtendaji wa Mtaa, Kata, ambayo yupo mtoto aliyenyimwa haki ya kwenda shule, ana miaka tisa pamoja na akili yote hiyo haendi shulena watendaji wametulia tulia wanasubiri ndugu wajitokeze nakuja Mwanza" alisisitiza Waziri Dkt. Gwajima
Amefafanua kuwa vitendo vya ukeketaji vinaweza kukomeshwa endapo wanaume watakaa katika makundi yao na kujadiliana jinsi ya kukomesha vitendo hivyo na kuongeza kuwa ukeketaji unaendelea kwa sababu wanaume hawajaamua kusema ukeketaji basi.
Awali akisoma taarifa ya Kituo cha Masanga kwa Mhe. Waziri, Meneja wa Mradi wa kupinga Ukeketaji Kituoni hapo, Valerian Mgani amesema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto ya bweni, chombo cha usafiri na watoto wa kike kukatishwa masomo, kukeketwa na kuozeshwa katika umri mdogo.
Ameongeza kuwa Kituo cha Nyumba salama cha Masanga kilianzishwa na mwaka 2006 na kusajili mwaka 2015 kwa lengo la kuwahudumia watoto wahanga wa ukatili ukiwemo ukeketaji ambapo hadi sasa kituo hicho kinahudumia walengwa 34 kati yao mmoja wa kiume.
Katika hatua nyingine, Waziri Dkt. Gwajima alitembelea Makao ya Watoto ya City of Hope yaliyoko katika shule ya Kumbukumbu ya Dkt. John Chacha inayojishughulisha na huduma kwa jamii ikiwemo kujenga miundombinu ya maji, kilimo, Makazi Bora na kuwasaidia watoto wanaotoka katika familia masikini kupata elimu ndani na nje ya nchi.
Post a Comment