Ads

GLOBAL PEACE FOUNDATION TANZANIA, UN WOMEN, SIMBA SPORTS, CHAMA CHA MPIRA WA MIGUU WANAWAKE TANZANIA, WADHAMILIA KUTOKOMEZA UKATILI WA KIJINSIA KWA WANAWAKE KATIKA SEKTA YA MICHEZO.

Wachezaji wa Simba Queens wakiwa katika picha ya pamoja na Afisa Mawasiliano na Mradi wa Global Peace Foundation Tanzania (GPF) Bi. Sylvia Mkomwa (aliyevaa t- shirt nyeusi)
Mkurugenzi mkazi wa Global Peace Foundation Tanzania (GPF) Bi. Martha Nghambi (katikati) akizungumza jambo katika maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani yaliofanyika leo ( Machi 9, 2021) jijini Dar es Salaam katika ofisi za GPF kwa kujadiliana mada ya namna gani wanaweza kutokomeza ukatili wa kinjisia kwa wanawake katika sekta ya michezo na jamii kwa jumla, katika maadhimisho hayo waliwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wachezaji wa mpira wa miguu wa Simba Queens kwa niaba ya wachezaji wote. 
Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) Bi. Amina Karuma wa pili kutoka kulia akizungumza jambo katika maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani yaliofanyika katika ofisi za Global Peace Foundation Tanzania (GPF) jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Klabu ya Simba (C.E.O) Bi. Barbar Gonzalez akiwapongeza baadhi ya wachangiaji wa mada ya namna gani wanaweza kutomeza ukatili wa kinjisia kwa wanawake katika sekta ya michezo na jamii kwa jumla katika maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani yaliofanyika leo ( Machi 9, 2021) jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wachezaji wa mpira wa miguu klabu ya Simba Queens wakishiriki katika maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani  kwa kushiriki mada ya namna gani wanaweza kutokomeza ukatili wa kinjisia kwa wanawake katika sekta ya michezo na jamii kwa jumla.
Mratibu wa Mtandao wa Ushirikishwaji Wanaume Bw. Idd Mziray.
Mtaalam wa Programu kutoka Chombo cha Umoja wa Mataifa katika usawa wa kijinsi na Uwezeshaji wa Wanawake (UN WOMEN), Bi. Lucy Tesha akichangia mada ya namna ya kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Raising Up Friendndiship Foundation, Bi. Hilda Ngasa 







..........................
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM 
Global Peace Foundation Tanzania, UN Women Tanzania, Simba Sports na Chama Cha Mpira wa Miguu Wanawake Tanzania wadhamilia Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake na Wasichana kwenye Michezo nchini Tanzania.

Hata hivyo imeelezwa kuwa uongozi wa klabu ya Simba kwa kushirikiana na Chombo cha umoja wa mataifa katika usawa wa kijinsi na uwezeshaji wa wanawake (UN WOMEN) wataandaa utaratibu wa kutengeneza mfumo wa kutoa taarifa za ukatili wa kijinsi kwa wachezaji wote wanawake ili kutokomeza ukatili wa kijinsia.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika majadiliano ya pamoja baina ya taasisi hizo wakiwemo wachezaji wa timu ya wanawake Simba Queens, Mkurugenzi mkazi wa Global Peace Foundation Bi. Martha Nghambi, amesema kuwa wapo katika kampeni ya kupinga na kutokomeza ukatili wa kijinsia katika nyanja mbalimbali ikiwemo mchezo wa mpira wa miguu kwa wanawake.

Bi. Nghambi amesema kuwa furaha yake ni kuona wanawake wanapigania haki zao, jambo ambalo litasaidia kufikia malengo ambayo yamekusudiwa katika kuhakikisha wanatokomeza ukatili ya kijinsia.

“Tutaendelea kuandaa programu mbalimbali zenye lengo la kuleta usawa katika jamii na taifa kwa ujumla” amesema Bi. Nghambi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Klabu ya Simba (C.E. O) Bi. Barbar Gonzalez, amesema kuwa lengo la kujadili kwa pamoja ni kuangalia namna wanavyoweza kutokomeza ukatili wa kijinsia katika sekta ya michezo kwa wanawake.

Bi. Gonzalez amesema kuwa kuna changamoto nyingi wanazopitia wanamichezo wanawake kufikia ndoto zao ikiwemo kukwamishwa na baadhi ya wanaume katika mazingira ambayo sio rafiki.

“Napenda kucheza mpira wa miguu, lakini sikukata tamaa kwa sababu ili kufikia ndoto zako unatakiwa kupambana pamoja na kuongeza juhudi kwa kile ambacho umekusudia kufanya kwa ubunifu” amesema Bi. Gonzalez.

Mratibu wa Mtandao wa Ushirikishwaji Wanaume Bw. Idd Mziray, amesema kuwa kuna mifumo ambayo ipo katika jamii ambayo imejengeka kuwa wanawake hawawezi kufanya kazi fulani kutokana na mazingira jambo ambalo sio kweli.

“Kuna wanawake tayari wanajiona hawawezi kufanya kazi fulani bila ya msaada kutoka kwa mwanaume kitu ambacho sio kweli” amesema Bw. Mziray.

Kocha msaidizi wa klabu ya Simba Queens Matty Diola, amelalamika kwa kuwepo unyanyasaji kwa wachezaji wa kike katika timu mbalimbali za mpira wa miguu kwa kile alichodai kuna ubaguzi katika ulipwaji wa posho kwa wachezaji wa kike na wa kiume.

"Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanaume wanalipwa posho kubwa tofauti na timu ya wanawake, naomba viongozi mlifanyie kazi" amesema Bi. Dialo.

Mtaalam wa Programu kutoka Chombo cha Umoja wa Mataifa katika usawa wa kijinsi na Uwezeshaji wa Wanawake (UN WOMEN), Bi. Lucy Tesha, amesema kuwa katika mchezo wa mpira wa miguu kwa wanawake kuna ukatili wa aina nyingi ikiwemo kutumia lugha za matusi, uku baadhi ya wachezaji  hawapewi nafasi ya kucheza mpaka watoe rushwa ya ngono.

Bi. Tesha ameeleza kuwa wapo baadhi ya wachezaji wakike wamekuwa wakikatishwa tamaa na wanaume kutokana na sababu ambazo kimsingi hazina maana yoyote na kushindwa kusonga mbele.

"Licha ya kuendelea kuripoti vizuri matukio ya ukatili wa kijinsia, naomba kila taasisi waweke mfumo wa kuripoti matukio hayo kwa ufanisi kwani itasaidia kutokomeza ukatili" amesema Bi. Tesha.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) Bi. Amina Karuma, amesema kuwa atazifanyia kazi changamoto zote ambazo zipo kwa wachezaji wa kike ambazo zinaonyesha ukatili wa kijinsia.

Bi. Karuma amewataka wachezaji wote waendelee kujituma na kufanya kazi kwa ufanisi na ubunifu jambo ambalo litawaletea mafanikio.

"Mikutano kama hii ya kuwakutanisha wadau mbalimbali itaendelea kufanyika ili tuweze kupokea mawazo ambayo yatatusaidia kutokomeza ukatili wa kijinsia" amesema Bi. Karuna.

No comments