Ads

Ilala Islamic Yaongoza Ufaulu bora kidato cha nne na sita:

SHULE ya Ilala Islamic ya jijini Dar es Salaam imejikita katika kuwaandaa vijana kuwa na maadili mema ndani ya jamii hatua inayopelekea kuweza  kupata matokeo bora.

Shule hiyo imeweza kufuta matokeo mabaya na kuweza kapata mafanikio makubwa kitaaluma ndani ya miaka 10 mfululizo ambapo haikuweza kupata matokeo ya daraja la tatu, nne na ziro.

Katika miaka mitatu ya mwisho kuanzia 2018 ,2019 na 2020 wahitimu wote wameweza kupata matokeo mazuri katika daraja la kwanza na la pili na kuifanya shule hiyo kuwa bora na inayofanya vizuri kitaaluma.

Ilala Islamic ni Shule ya bweni na kutwa inayosimamia misingi bora ya dini ya kiislamu kwa kuwafundisha vijana  namna ya kushiriki vema katika shughuli mbalimbali za kitaifa na zile za kidini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Msimamizi Mkuu wa shule hiyo Mohammed Akida amesema mafanikio ya malengo waliyoyaweka yameweza kufikiwa  kwa asilimia mia moja kiasi ambacho Uongozi wa shule hiyo umekuwa ukijivunia.

Amesema mwaka 2020/21 shule hiyo imeweza kupata matokeo bora ambapo wanafunzi 36 walipata daraja la kwanza na sita kupata daraja la pili hata hivyo hapakuwa na daraja la tatu, nne na Ziro kitu kilichoifanya shule hiyo kushika nafasi ya 9 kimkoa na 80 kitaifa katika zaidi ya Shule elfu 5.

Msimamizi huyo ameelezea juhudi zao ndizo zilizopelekea kujipatia tunzo kutoka kwenye taasisi mbalimbali  ambapo mwaka 2016 waliweza kupata tunzo katika mashindano ya kawaida ya Ramadhani Quiz pamoja na yale ya Wizara ya elimu, kwa shule binafsi shule hiyo ilishika nafasi ya nne pia ikaja kushika nafasi ya tatu, ya kwanza sambamba na kukamata nafasi ya pili ndani ya miaka saba mfululizo.

Aidha shula ya kiislamu ya Ilala iliweza kushiriki na kuweza kushinda kwenye mashindano ya kuongea lugha ya kiingereza yaliyoshirikisha shule zote za Sekondari za jiji la Dar es Salaam.

Anaendelea kuwa malengo makubwa ya Shule hiyo ni kuhakikisha wanafunzi wanapata ufaulu mzuri katika masomo ya dini na masomo mengine sambamba na kuhifadhi kitabu cha dini ya kiislamu na kuijenga jamii ya vijana hao kuwa wenye kuwatumikia wengine.

"Kama uongozi tumeweka mikakati ya kuhakikisha shule yetu inafanya vizuri na wanafunzi wanapata ufaulu mkubwa katika masomo ya dini na mengine ikiwemo kuhifadhi juzu katika kitabu cha Kur aan," amesema Akida.

Amesema sambamba na hilo ameeleza wanapenda kuona vijana wengi wanaendelea kusoma kwenye Vyuo mbalimbali vilivyoko hapa nchini na nje kitu kitachopelekea kuongezeka kwa wataalamu mbalimbali kwenye sekta ya afya,uhandisi na wajasiriamali wakiwemo wataalamu wa kilimo,ufugaji.

Katika kulitambua hilo shule hiyo iliongeza juhudi katika kuongeza mbinu za ufundishaji ili kuinua kiwango cha elimu katika shule hiyo ambapo mwaka 2020/21 imeshika nafasi ya 80 kitaifa kutokana na jitihada za kuwapa mazoezi na mitihani kama njia ya kuwajengea uwezo.

Aidha amesema ujuzi na maarifa ni vitu vinavyopewa kipaumbele katika kutimiza mipango shule hiyo kitaaluma ili kuweza kupata daraja la kwanza katika matokeo ya kidato cha nne na kufanya vizuri zaidi katika ufaulu wa kidato cha sita.

Kwa upande wa malezi Mkuu huyo amesema shule hiyo ina mazingira bora na salama kwa vijana wa kike na wakiume kiasi ambacho mkubwa kumuheshimu mdogo na mdogo kumuheshimu mkubwa ni utaratibu uliokuwepo katika shule hiyo.

"Shule yetu imekuwa ikiwapatia vijana malezi bora yaliyo katika misingi ya dini ya kiislamu lwa kuzingatia namna ya kujihifadhi,kula na kuongea pale panapo hitajika," amesema Mkuu huyo.

Kwa upande wake makamu wa utawala wa shule hiyo Rashidi Mohammed amesema shule yao ni kitovu cha mafanikio kwa wanafunzi wanaosoma kozi mbalimbali.

Amesema nidhamu ni kitu cha msingi kinachowawezesha kufikia malengo waliyojiwekea hata hivyo wanakwenda kinyume na utaratibu wa sheria za shule huchukuliwa hatua za kinidhamu.

Wanafunzi wengi wanaosoma katika shule hiyo wamekuwa na ndoto za kufika mbali ili kufanikisha azma ya malengo na mikakati ya kupata ufaulu wa kiwango cha daraja la kwanza.

"Wanafunzi wanaosoma katika shule hii wana ndoto ya kuwa madaktari,wauguzi,wahandisi na walimu wa dini ya kiislamu pia tuna maabara yenye vifaa vya kujifunzia kwa masomo ya sayansi kwa vitendo ili waweze kutimiza malengo yao," amesema Mohamed

Makamu huyo amesema wanawafundisha wanafunzi kwa kujitoa yaani wanawachukulia kama watoto wao ili kuwatimizia ndoto walizonazo pindi watakapo maliza masomo yao pia wako tayari kuwafundisha kupitia muda wa ziada ilimradi waweze kufaulu.

Anamalizia kwa kusema kwamba Shule hiyo inazingatia nidhamu ya mavazi kwa watumishi na wanafunzi hivyo amewaomba wazazi na walezi kuwapeleka watoto wakapate elimu shuleni hapo. 

No comments