GLOBAL PEACE FOUNDATION TANZANIA KUHAMASISHA AMANI MKOA WA MTWARA
Global Peace Foundation Tanzania (GPF ) kwa kushirikiana na Shirika la Tanzania Building Future (TABUFO) wameanza kutekeleza mradi wa pamoja wa Amani Yetu; Uhai Wetu ambao umekusudia kuimarisha uelewa wa jamii na kuchagiza ushiriki wao katika ujenzi wa amani, utatuzi wa mizozo na kuzuia vurugu za itikadi kali.
Mradi huo unatekelezwa katika kata ya Nanguruwe na Msimbati, Manispaa ya Mtwara Vijijini Mkoa wa Mtwara.
Akizungumzia utekelezaji wa maradi huo, Mkurugenzi Mkazi wa Global Peace Foundation Bi. Martha Nghambi, amesema kuwa utekelezaji wa mradi katika shughuli ya kwanza ilifanywa Januari 14 hadi 18 mwaka huu, ambapo kwa muda wa siku mbili walitoa elimu pamoja na kupata mabalozi wa amani katika vijiji.
“Katika vijiji vinne vya Kata ya Msimbati na vijiji vitano vya kata ya Nanguruwe kila kijiji kilitoa wawakilishi wawili; na siku mbili zilizobaki tulitoa mafunzo maalum ya ujenzi wa amani, utatuzi wa mizozo na kuzuia vurugu za itikali kali”amesema Bi. Nghambi.
Amesema kuwa washiriki 24 walihudhuria mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa TCCIA huko Mtwara, kuanzia Februari 11 hadi 12 mwaka.
“Madhumuni ya mafunzo ni kuwajengea uwezo viongozi wa kijamii na wadau wakuu wa amani katika jamii ikiwa ni pamoja na kukuza uelewa wao juu ya amani, ujenzi wa amani, utatuzi wa migogoro na kuzuia vurugu za itikadi kali ” amesema Bi. Nghambi.
Amefafanua kuwa katika mradi huo wamefanikiwa kufungua klabu za amani za vijana katika Shule ya Msingi na Sekondari ya Msimbati, Nanguruwe.
Ameeleza kuwa Januari 23 hadi 27 Januari 2021 GPF Tanzania na TABUFO walifanya vikao vya kuhamasisha na kufungua rasmi klabu hizo ambapo zoezi hilo lililenga kuwawezesha wanafunzi 60 waliochaguliwa kuchukua jukumu kuwa mabalozi wa amani kwa kushirikiana walimu wao.
Ameeleza kwa miezi 12 ijayo, mabalozi wa amani kutoka vijijini waliopewa mafunzo na viongozi wao na wanafunzi waliopewa mafunzo wataendelea kutekeleza mipango anuwai ya kuhamasisha ushiriki wa jamii katika ujenzi wa Amani, kutatua migogoro na kuzuia vurugu za itikadi kali.
Post a Comment