UDOM kudahili Wanafunzi 12,000, Wazazi wasisitizwa kuwapeleka wanafunzi kujiunga na kozi mbalimbali.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha UDOM Taaluma,Utafiti na Ushauri Profesa Alexander Makulilo akiwa mbele ya Banda la kutolea maelezo lililopo kwenye maonesho ya 15 ya Vyuo Vikuu ,Viwanja vya Mnazi Mmoja.
..............................................
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimesema katika Mwaka wa Masomo wa 2020/21 kitahadili wanafunzi 12,000 watakaojiunga na programu mbalimbali za masomo zinazotolewa na chuo hicho.
Aidha, kimewasisitiza wazazi kuchangamkia fursa za kozi za masomo zinazofundishwa chuoni hapo kwa wanafunzi kwani kina miundo mbinu bora ya kujifunzia ikiwemo hosteli za kutosha, maktaba yenye ubora pamoja na wahadhiri wa kutosha katika masomo chuoni hapo.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Naibu Makamu Mkuu wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Udom Profesa Alexander Makulilo katika Maonyesho ya Elimu ya Juu ,Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) yanayoendelea Viwanja vya Mnazi Mmoja.
Alisema kuwa chuo kwa sasa kina wanafunzi 30,000 wa kozi mbalimbali ambapo uwezo wake ni kuchukua 40,000 na kubainisha mwaka huu wa masomo watadahili wanafunzi 12,000.
" Chuo hiki kwa sasa ni cha kwanza kwa ukubwa Afrika Mashariki, hivyo kina uwezo wa kudahili wanafunzi wengi wa program tofauti mwaka huu tunategemea kudahili wanafunzi wengi," alisema Profesa Makulilo.
Alibainisha kuwa kutokana na ubora wa utoaji elimu kwenye kozi za chuo hicho, hivyo ni sehemu sahihi wazazi kuwashauri watoto wao waliohitimu kidato cha sita kuchagua kozi mbalimbali za kujiunga na chuo.
Alifafanua kuwa UDOM kina Shule saba zinazofundishwa katika program za masomo tofauti ya Shahada zaidi ya 80 ikiwemo ndaki ya elimu, Insia na sayansi za jamii, sayansi za ardhi na uhandisi.
Ndaki nyingine ni sayansi za mawasiliano na mifumo ya kompyuta, sayansi asilia na hisabati pamoja na sayansi za afya
Post a Comment