Chuo cha Mipango cha Mipango ya Maendeleo Vijijini champongeza JPM kufika Uchumi wa Kati, Chajipanga kujenga Kiwanda cha Barafu
Msajili wa Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Mkoani Dodoma Profesa Mwabless Malila akizungumza na wanahabari katika Maonyesho ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
...........
Chuo Kikuu cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kimempongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa kuifikisha nchi katika uchumi wa kati kabla ya kufika mwaka 2025.
Chuo hicho kimesema kitajenga Kiwanda cha Barafu Kanda ya Ziwa kitakachowanufaisha wavuvi wanaopatikana ukanda huo pamoja na kuwainua kiuchumi.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Chuo hicho Profesa Hozen Mayaya katika Maonesho ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) yanayofikia kilele kesho Viwanja vya Mnazi Mmoja.
Alisema Rais Magufuli kuivusha nchi hadi kwenye uchumi wa kati inaonyesha kuwa ni kiongozi anayejali maisha ya wananchi wake na maendeleo kwa ujumla.
" Nampongeza Rais Magufuli kutufikisha katika uchumi wa kati inaonyesha tuna kiongozi madhubuti tunamuomba Mungu aendelee kumpatia moyo wa kuwapigania wananchi ," alisema Profesa Mayaya.
Alibainisha kuwa ni jambo jema nchi kuifikia uchumi huo na kwamba chuo hicho kinashiriki katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo (2023-2026) ambapo kitajikita katika kuangalia masoko ya bidhaa.
Alisisitiza kuwa kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo Duniani (UNDP) watajenga kiwanda hicho lengo likiwa kuwarahisishia wavuvi kuhifadhi samaki na kuwainua kimapato.
Aliongeza kuwa mbali na mradi huo tayari chuo kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) kilijenga kiwanda cha ngozi pamoja na Mradi wa kuwaongezea thamani wakulima wa vitunguu swaumu, Mbulu.
Mkuu wa chuo huyo aliwahimiza wakazi wa kanda hiyo kulima viazi lishe ili kujikwamua kiuchumi na kujiongezea kipato.
Profesa Mayaya alisema licha ya kufundisha kozi za mrefu na fupi wanajihusisha na ufanyaji tafiti, utoaji ushauri wa Mipango ya Maendeleo ikiwemo ya ardhi.
Aliwahimiza wazazi na wahitimu wa kidato cha sita kuchangamkia fursa ya program za masomo zinazotolewa chuoni hapo ili nchi ipate wataalamu wengi waliobobea katika Mipango mbalimbali ya Maendeleo.
Kwa upande wake Msajili wa chuo hicho mkoani Dodoma Profesa Mwabless Malila alisema wanashiriki maonyesho hayo lengo likiwa kutangaza huduma zao na kubainisha wanatoa kozi mbalimbali kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada ya uzamili.
Pia alisema chuo hicho katika kuhakikisha kinawakomboa wananchi na umaskini kilifanya tafiti mbalimbali ikiwemo ya Eco-Village katika Kijiji cha Chilolo mkoani ambapo wanakijiji walisaidiwa kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi hali iliyochangoa kupata chakula cha kutosha.
Post a Comment