Wakulima wa Ufuta Nchini Wauza na Kujipatia Shilingi Bil 8.7
Naibu katibu Mkuu Wizara ya Kilimo (kulia) akiwa na mtaalam kutoka Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) wakikagua shughuli za upokeaji zao la ufuta.
SOKO la Bidhaa nchini limefanya minada miwili iliyojumuisha mauzo ya zao la ufuta lenye jumla ya tani 6137 zenye thamani ya shilingi Bilioni 9.3 ambapo shilingi Bilioni 8.7 zilienda kwa wakulima.
Hali nchini tangu kuanza ununuzi wa mazao ya wakulima kupitia soko hilo limekuwa likilenga kuongeza ufanisi katika mifumo ya masoko iliyo na changamoto kwa kuwaunganisha wauzaji na wanunuzi wa bidhaa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwisho wa wiki iliyopita Dar es Salaam Afisa Mwandamizi Uendeshaji Biashara wa Soko la Bidhaa nchini (TMX) Nicolaus Kaserwa alisema soko hilo wiki iliyopita lilifanya Minada miwili iliyojumuisha tani 6137 yenye thamani ya shilingi Bilioni 9.3.
Alisema katika kufanyika huko Shilingi Bilioni 8.7 zilienda kwa wakulima na shilingi milioni 299 ikiwa ni ushuru wa halmashauri za Wilaya.
"Mnada uliofanyika juni 23 ulijumuisha Mkoa wa Mtwara na Pwani ambapo jumla ya kiasi (Volume)kilichowekwa kwa ajili ya mauzo katika mnada huo ilikuwa ni Tani 5,692," alisema Nicolaus.
Alisema kati ya tani hizo ,tani 4,246 ziliuzwa na wakulima waliridhia bei iliyopatikana sokoni ambapo bei ya juu ilikuwa ni shilingi 1,791.
Aidha alisema kuwa katika mauzo hayo fedha inayoenda kwa wakulima ni shilingi Bilioni 6.7 na ushuru wa halmashauri ni shilingi milioni 230.
Pia alisema kuwa mnada uliofuatia ukijumuisha mikoa ya Dodoma na Mtwara ilikuwa Juni 24 ambapo tani 1,345 zenye thamani ya shilingi bilioni 2.1 .
Aliongeza kuwa fedha hizo zikijumuisha tani 900 za Mkoa wa Mtwara ambazo hazikuuzwa kwenye mnada wa Juni 23 ziliuzwa tena kwenye mnada huo,bei ya jumla iliyopatikana ilikuwa ni shilingi 1,793 katika mauzo hayo.
"Katika mauzo hayo ,shilingi bilioni 2 zilienda kwa wakulima na milioni 69zililipwa ikiwa ni ushuru wa halmashauri za Wilaya husika," alisema Nicolaus.
Tayari serikali imeisha sema kuwa mfumo huo utawahakikishia wakulima upatikanaji wa malipo kwa muda mfupi wa wanunuzi kuwa na uhakika wa kupata mazao na bidhaa zenye ubora na zinazotosheleza mahitaji yao.
Kuanza kufanyika kazi kwa mfumo huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ibara namba 22 (g) (ii) miaka mitano 2016 hadi 2017 na 2021.
Katika hatua hiyo serikali imekuwa inasimamia utekelezaji wa Blue Print iliyo lenga kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini.
Post a Comment