Waziri wa Kilimo Akagua Kituo cha Ununuzu wa Mahindi cha Kizuka, Mkoani Ruvuma
WAZIRI
wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amefanya ziara ya ukaguzi katika
Kituo cha Ununuzu wa Mahindi cha Kizuka, Mkoani Ruvuma tarehe 18
Septemba 2024.
Akiongea
na wakulima waliokuwa wanachekecha na kuchambua mahindi katika Kituo
hicho, Waziri Bashe amewaeleza wakulima hao kuwa Serikali ya Awamu ya
Sita ni sikivu na imeweka kipaumbele katika kutatua changamoto zozote
walizonazo kabla ya msimu wa mvua kuanza.
Wakulima
kadhaa walieleza changamoto zao wakiwemo Bw. Nicodem Mayo, Bi. Zena
Zawamba, Bw. Paul Philemon Haule na Baltazari Komba Mjinga, ambao
wamevuna magunia zaidi ya 330 kwenye mashamba ya hekari 15 wameomba
mawakala wanunue mahindi vijijini kwa angalau shilingi 600 hadi 650
badala ya shilingi 350 ambayo ni hasara kwa wakulima. Pia wameomba
miundombinu ya barabara na mawasiliano kutengenezwa, mashine za kisasa
kuchambua mahindi, kuongezewa huduma za maafisa ugani na zana za kilimo
na mbegu bora.
Akijibu
changamoto kadhaa, Waziri Bashe ameeleza kuwa “nimeona uhitaji wa kuwa
na mashine ya kisasa ya kuchambua na kusafisha mahindi. Nimeielekeza
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kununua mashine za kisasa
za kuchambua mahindi ili kurahisisha huduma za Kituo hicho kwa
wakulima,” amesema Waziri Bashe.
Aidha,
amemuomba Mkuu wa Wilaya Mhe. Wilman Kapenjama Ndile kutembelea
mawakala wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na kuhakikisha
wananunua mahindi kwa wakulima kwa shilingi 700 kwa kilo. “Vinginevyo,
waende kununua mahindi NFRA moja kwa moja,” ameongeza Waziri Bashe.
Wakulima
hao pia wameelezwa kuwa wataongezewa maghala ya kuhifadhi chakula,
mizani ya kidigitali, kujengewa Kituo cha Zana za Kilimo, kupatiwa mbegu
za mahindi za ruzuku zikiwemo aina ya Hybrid na OPV, pamoja na mbolea
za ruzuku. Kuhusu miundombinu ya barabara na mawasiliano, Waziri Bashe
ameeleza ataongea na viongozi wa sekta husika kwa ajili ya kusaidia ili
kuongeza tija kwa wakulima.
Awali, Waziri Bashe alitembelea pia ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed ambapo ameridhia ombi la Mkuu wa Mkoa kutumia shamba la Tumbaku la Ruvuma kuwa shamba la BBT kwa ajili ya matumizi ya wakulima waliopo karibu nalo.
Post a Comment