Ads

SERIKALI KUANZA KUGAWA MABAHEWA KWA WAFANYA BIASHARA






SERIKALI kupitia Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano imesema inatarajia kuanza mchakato wa kugawa mabehewa yanayomilikiwa na Shirika la Reli Tanzania(TRC) kwa wafanyabiashara wakubwa na wakati ambao watayahitaji kuyatumia kusafirisha shehena ya mizigo yao kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Kwa mujibu wa Wizara hiyo kwa sasa kuna mabehewa zaidi ya 1,000 ambayo yatatolewa kwa wafanyabiashara ambapo watatakiwa kuyafanyia matengenezo na kisha kuanza kuyatumia kusafirisha shehena za mizigo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo  Desemba 14 mwaka 2019 katika  Bandari ya Kemondo Bay iliyopo mkoani Kagera, Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Issack Kamwelwe amesema mchakato huo wa kutoa mabehewa utaanza baada ya kufanyika kikao kati yake na wadau na hasa wafanyabishara wanaotumia usafiri wa meli na reli kusafirisha mizigo yao kati ya eneo moja na jingine.

Mhandisi Kamwelwe ameongeza mabehewa hayo ambayo watapewa wanaoyahitaji licha ya kuyafanyia matengenezo kwa fedha zao bado yatabaki kuwa Mali ya Shirika la Reli Tanzania(TRC), kwa maana chini ya umiliki wa Serikali."Mabehewa ambayo tunayo pale TRC tutawapa wafanyabiashara na sisi tutawaruhsu kutumia miundombinu ya reli lakini tutakuwa tukipata ushuru unaotokana na kutumia reli.

"Hivyo kati ya siku mbili hizi nitakuwa na kikao na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania(TRC), Mhandisi Masanja Kadogosa ili kujadili kwa kina suala hilo ambalo sasa litatufanya turahisishe utoaji wa huduma za usafiri.Tunaka tukimbie badala ya kuendelea kwani imetuchelewesha sana,"amesema  Waziri Kamwelwe.

Amesema  utaratibu huo wa kutumia mabehewa ukianza utamuwezesha mfanyabishara husika kuwa na uhakika wa kusafirisha mzigo wake wakati wowote kwani atakuwa na mabehewa yake mwenyewe ambayo anayahudumia na kazi ya TRC itakuwa kutoa kichwa cha treni kuvuta behewa ambazo zikifika katika bandari behewa litaingia kwenye meli maalum ambayo nayo ina njia za reli ambazo zinabeba behewa hizo.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk.John Magufuli imedhamiria kwa dhati kuboresha huduma muhimu kwa wananchi na katika eneo la maziwa makuu kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Kampuni ya Huduma za Meli kuna uteketezaji mkubwa wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya bandari ,gati, ujenzi wa reli katika bandari zinatumika kubeba mizigo, ujenzi wa meli mpya pamoja na kufanya matengenezo makubwa ya meli za zamani ambapo miradi hiyo lengo lake ni kuboresha huduma ya usafiri wa majini.

Hata hivyo, akiwa bandari ya Kemondo amekutana na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wanaotumia bandari hiyo pamoja na Bandari ya Bukoba wametoa ombi la kuangalia upya kwa gharama za ushuru wa bandarini ambao ni mkubwa uliongezwa siku za karibu ambapo Waziri amesema atayafanyia kazi yote ambayo yameelezwa kwani nia ya Serikali ni kutoa huduma katika mazingira rafiki.

No comments