TANTRADE YASAIDIA KAMPUNI 31,891 KUPATA TAARIFA ZA BEI YA MASOKO NA BIDHAA
Na Mwandishi Wetu,
Mwamba wa habari
MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara
Tanzania (TANTRADE) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Serikali ya
Awamu ya Tano imefanikiwa kuziunganisha kampuni 31,891 kuweza kupata taarifa za
bei na masoko ya bidhaa za ndani na nje
ya nchi.
Hayo yamebainishwa leo Jumatano
(Novemba 27, 2019) Jijini Dar es Salaam na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE,
Latifa Khamis wakati alipokuwa akitoa taarifa ya mafanikio ya Taasisi hiyo
katika Kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano kuanzia
Novemba 2015 hadi Novemba 2019.
Alisema kuwa ya wafanyabiashara
hao, TANTRADE iliweza kuunganisha katika masoko wafanyabiashara 405 na kuuza tani 102,000 za mahindi, tani
2,000 za karanga, tani 5,000 za soya, tani 50 za ufuta, tani 7 za majani ya
papai, kilogramu 200 za unga wa ubuyu, tani 2 za iliki, tani 5,000 za muhogo na
tani 3.2 za tangawizi ya unga.
Aliongeza kuwa miongoni mwa
bidhaa zilizoonesha uhitaji mkubwa katika masoko ya nje ni pamoja na matunda, samaki
na mazao ya bahari, jamii ya mikunde, asali, kahawa, chai, korosho, viungo na
vyakula, ambapo maulizo ya bidhaa hizo yalitoka katika nchi za India, Nchi za
Kiarabu, Misri, Marekani, Vietnam na Ulaya.
‘’Mbali na kusambaza taarifa za
uhitaji wa bidhaa mbalimbali TANTRADE kwa kushirikiana na wanunuzi kutoka nchi
zao tumewezesha kupatikana kwa muendelezo wa kimkakati wa kupenya katika masoko
yao, semina mbalimbali ziliratibiwa ambapo wafanyabiashara na wadau 425
walishiriki ili kutambua fursa za masoko ya nje na taratibu za kuyafikia’’ alisema Latifa.
Kuhusu ukuzaji na uendelezaji wa
masoko ya nje ya nchi, Latifa alisema TANTRADE imeendelea kuratibu maonesho ya
biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) kwa lengo la kutoa fursa za
kutangaza bidhaa zilizoongezewa thamani na upatikanaji wa teknolojia ili
kupanua wigo wa masoko ya nje ya nchi.
Latifa alisema kupitia DITF kila
mwaka Tanzania hupokea wastani wa kampuni 500
kutoka zaidi ya nchi 35 zinazoshiriki maonesho hayo na hivyo kuwasaidia
wafanyabiashara katika upatikanaji wa teknolojia na kusaidia kutatua changamoto
za uzalishaji hafifu wa bidhaa za kilimo, uchenjuaji wa madini na hivyo kuleta
matokeo chanya yaliyokusudiwa.
Akifafanua zaidi Latifa alisema kwa
mwaka 2019 pekee kupitia DITF, mafanikio mbalimbali yaliweza kupatikana ikiwemo
kampuni 437 kupata oda ya kufanya biashara zenye thamani ya Tsh Bilioni 7.93,
kufanyika kwa mauzo ya papo kwa papo yenye thamani ya wastani wa Tsh. Milioni
209, pamoja na kutengeneza ajira za muda mfupi zipatazo 14,912 zilizotokana na
kazi mbalimbali za maonesho ikiwemo ujenzi, ulinzi na usafi.
Akizungumzia kuhusu ushiriki wa
Tanzania katika maonesho ya nje ya nchi, Latifa alisema Tanzania imefanikiwa
kushiriki katika maonesho katika nchi zilizo na utengamano ikiwemo Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika
(SADC) ambapo wastani wa kampuni 200 zimeweza kushiriki na kutambua bidhaa zao
kwenye nchi hizo na kuingia mikataba ya kibiashara ili kupata masoko endelevu.
Akitoa mfano Latifa alisema
katika mwaka 2018/19, Tanzania ilishiriki maonesho ya 15 ya Biashara China
ambapo kampuni 20 zilishiriki na kuweza kutafutiwa masoko ya bidhaa na
kutangaza vivutio mbalimbali vya uwekezaji ikiwemo vivutio vya utalii, mazao ya
kilimo hususani kahawa, chai, karafuu, asali, korosho, mazao ya jamii ya kunde
na bidhaa za mikono ikiwemo vikoi.
‘’Katika maonesho ya chakula ya
Gulfood-Dubai kampuni tatu zaTanzania zilifanikiwa kutembelea maonesho hayo
yaliyofanyika Dubai kwa lengo la kutambua fursa mbalimbali kutoka kwa
washiriki, ambapo wanunuzi wa bidhaa mbalimbali kama asali kontena 30, kahawa
tani 50, ukwaju tani 10 walipatikana’’ alisema Latifa.
Aidha Latifa alisema TANTRADE
katika kutekeleza adhima ya Tanzania ya Viwanda ilianzisha maonesho ya bidhaa
za Viwanda vya Tanzania yanayofanyika kila mwezi Desemba, ambapo tangu kuanza
kwake mwaka 2007 wastani wa makampuni 497 hushiriki na kuwafanya wazalishaji wa
bidhaa nchini kupata fursa ya kutambulisha bidhaa zao na kuhamasisha matumizi
ya bidhaa za Tanzania.
Post a Comment