Mpinzani wa Bondia Mwakinyo atua leo Dar.
Bondia Arnel Tinampay anatarajia kuwasili leo nchini kuanzia majira saa 6.30 Mchana ambapo atapiga kambi ya siku 10 jijini Dar es Salaam kabla ya kumkabiri Hassan Mwakinyo.
Tinampay na Mwakinyo watazichapa Novemba 29 pambano la raundi 10 la uzani wa super welter litakalopigwa kwenye uwanja wa Uhuru Dar es Salaam huku rais John Pombe Magufuli akiombwa kuwa mgeni rasmi.
Mapema wiki iliyopita, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa bungeni mjini Dodoma aliwaomba watanzania kujitokeza kwa wingi kumsapoti Mwakinyo katika pambano hilo lililobeba hisia za wadau mbalimbali wa michezo ndani na nje ya nchi.
Tinampay anatarajiwa kuwasili nchini Leo Jumatatu na ndege ya Shirika la Ethiopia tayari kwa pambano hilo hilo litakalopigwa kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Akiwa nchini, bondia huyo ambaye ameambatana na kocha wake, Victor Man 'On fire' atafanya mazoezi ya wazi jijini Dar es Salaam kabla ya kuelekea Tanga, ambako atafanya kwenye uwanja wa Tangamano na kisha kurejea Dar es Salaam kumkabiri Mwakinyo.
Bondia huyo ambaye ni namba moja kwa ubora nchini Philippines kwenye uzani wa super welter tayari ameanza safari ya kuja Tanzania ambapo atawasili jijini Dar es Salaam Jumatatu.
Bondia huyo ametamba kumpiga kwa Knock Out, Mwakinyo katika ardhi ya Tanzania akisisitiza kuwa anafahamu ubora wa Mtanzania huyo ambao amesema ana punchi nzito.
"Nimejiandaa kushinda, nitajaribu kumpiga kwa KO mpinzani wangu, lazima nikashinde Tanzania," alisema Tinampay muda mfupi kabla ya kuanza safri ya kwenda Tanzania.
Promota wa pambano hilo, Jay Msangi amesema Tinampay atakapowasili atafanya mazoezi ya wazi Mlimani City na Mbagara jijini Dar es Salaam kabla ya kuelekea Tanga ilipo kambi ya Mwakinyo ambako pia atafanya mazoezi ya wazi kisha kurejea Dar es Salaam tayari kwa pambano.
"Maandalizi ya pambano yanakwenda vizuri ikiwa ni pamoja na Tinampay kuwasili leo jumatatu jijini Dar es Salaam," amesema Msangi.
Hivi karibuni akiwa Bungeni mjini Dodoma, Waziri Mkuu alizungumzia pambano hilo akitaka Watanzania kujitokeza kumsapoti Mwakinyo atakapokuwa akimkabiri bondia huyo kutoka Philippines.
Post a Comment