Ads

Bilal Muslim Mission yafanya Matembezi ya amani kumuenzi Imam Hussein na kuchangia damu



Jumuiya ya Bilal Muslim Mission  imefanya Matembezi ya amani ya Kumbukumbu ya kumuenzi na kuomboleza kifo cha Mjukuu wa Mtume Muhamad (SAW), Imam Hussein aliyeuawa kikatili huko mji wa Kerbala nchini Iraq na Jeshi la Yazid.
Aidha Jumuiya hiyo kwa kushirikiana Kikundi Marafiki kinachojihusisha na utoaji wa huduma za afya bure cha Maisha Njema Foundation pamoja na Mpango waTaifa wa Damu Salama-Kanda ya Mashariki na Pwani imeendesha kampeni ya uchangiaji damu ili kusaidia watu wenye mahitaji.
Akizungumza na wanahabari jana jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa  jumuiya hiyo, Hussein Karim alisema matembezi hayo yamefanyika ili kudumisha mwendelezo wa alama ya kuigwa iliyoachwa na kiongzi huyo ikiwemo kupinga dhuluma, unyanyasaji na udhalimu.
“ Tunafanya matembezi tumkimuenzi Imam Hussein alipinga udhalimu maombolezo yanaendana na uchangiaji damu hapa tulipo tutaendelea kutoa huduma za afya bure,” alisema Karim.
Alibainisha kuwa Jumamosi iliyopita jumuiya hiyo ilichangia chupa 600 za damu na kwamba Septemba 21 na 22 mwaka wataendesha kambi ya afya ambapo huduma mbalimbali za afya zitatolewa bila malipo.
Alisisitiza kuwa jumuiya hiyo  inaendelea na utoaji wa huduma jamii ikiwemo utoaji wa elimu na afya huku akibainisha wao ndio wanaochangia damu kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande daktari Dayynah Karim kutoka Maisha Njema Foundation alisema kikundi hicho katika utoaji huduma za afya kinashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Kampuni ya ulinzi ya G1, Mohamed Enterprises na Beta Foundation-Uingereza
Daktari Dayynah alisema wanatarajia kukusanya chupa 200 hadi 400 za damu na kwamba kambi ya afya itatoa huduma za uchangiaji damu, huduma za macho, huduma za meno, upimaji wa presha na sukari.
Alifafanua kuwa kambi hiyo si mara ya kwanza kuwekwa bali ilishawekwa kwenye mikoa ya Tanga, Kigoma na  Kigamboni-Dar es Salaam.

Kabla ya maandamano hayo Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama- Kanda ya Mashariki na Pwani iliendesha Kampeni ya Kuhamasisha Uchangiaji Damu kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Ashura ili kupunguza tatizo la upatikanaji wa damu hospitali.
 

No comments