Ads

WAFANYABIASHARA WALEMAVU WAMPONGEZA MEYA , MKURUGENZI ILALA KWA KUTATUA MGOGORO WA KODI.

Meya wa Manispaa ya Ilala Mhe. Omary Kumbilamoto.

Wafanyabiashara Walemavu wa Amana kwa Maasai wameshukuru na kuwapongeza Meya wa Manispaa ya Ilala, Omari Kumbilamoto na Mkurugenzi wa  Manispaa hiyo, Jumanne Shauri kwa kumaliza kutatua mgogoro wa kodi  ya fremu iliyokuwa imependekezwa wailipe kwa manispaa hiyo.

Awali wafanyabishara hao walikuwa wakilipa Sh elfu 30 lakini manispaa hiyo ilileta pendekezo jipya la kuwataka kulipa Sh elfu 80 hali iliyosababisha mgogoro kati yao na manispaa na kuwalazimu viongozi hao pamoja watendaji kukaa nao na kujadiliana kufikia mwafaka wa kulipa Sh elfu 50.

Shukrani na pongeza hizo wamezitoa jijini Dar es Salaam baada kukamilika utiaji saini wa mkataba mpya uliosainiwa na Meya Kumbilamoto katika Ofisi za manispaa hiyo.

Akizungumza na wanahabari jijini humo Mfanyabishara Subira Mwengoka alisema awali walikuwa wakilipa Sh elfu 30 ila walishangaa kuletewa pendekezo la kulipa Sh elfu 80 na kusababisha kutoelewana na manispaa hali iliyowalazimu kutafuta suluhu ya mgogoro huo na mwishowe walikubaliana kulipa Sh elfu 50 kama mkataba walioingia unavyoelekeza.

“ Tuliletewa pendekezo la kulipa Sh 80  na manispaa kiukweli ilitupa ukakasi kulipa nashukuru na nawapongeza  meya na mkurugenzi kwa kutukubalia kulipa Sh elfu 50,” alisema Subira.

Aliwahimiza wafanyabiashara wenzake kuunda vikundi kuchangamkia fursa ya asilimia 10 ya mikopo inayotolewa na manispaa kwa vijana, wakinamama na walemavu.

Mfanyabiashara Mlemavu wa Macho, Juma Malecha aliwashukuru na kuwapongeza viongozi kwa kusikia kilio chao kwa kukubali kuwapunguzia kiwango cha mpya iliyokuwa imependekezwa na kusisitiza kuwa halmashauri imekuwa mfano wa kuigwa  ya kuwasikiliza wafanyabiashara huku akiziomba halmashauri nyingine kuiga kutoka Ilala.

Meya wa Manispaa hiyo, Kumbilamoto alisema mgogoro huo umedumu kwa miezi minne na kwamba walipendekeza wafanyabiashara walipe Sh elfu 80 lakini kiwango hicho kiliibua mgogoro kusababisha yeye, mkurugenzi na watendaji kufanya majadiliano na kufikia makubaliano walipe Sh elfu 50.

Meya kumbilamoto alimshukuru na kumpongeza mkurungenzi wa manispaa hiyo kwa kukubali Wafanyabiashara hao kulipa kodi ya kiasi hicho cha fedha na kwamba mkataba walioingia ndio unaotakiwa kufuatwa.

Alisisitiza kuwa utatuzi wa mgogoro unaonyesha ni kwa jinsi gani mkurugenzi na watendaji wa manispaa hiyo wanavyotekeleza na kuunga mkono kauli ya Rais Dkt. John Magufuli inayowataka viongozi kuzitatua na kuzipatia ufumbuzi kero za wananchi.

Aliwakumbusha walemavu kujiungakatika vikundi vitakavyowasaidia kupata fursa za  mikopo inayotolewa na manispaa kwa kundi hilo.
Naye Mhasibu ambaye pia ni Msimamizi wa Mapato wa Maeneo ya Wazi, Salome Mdendu mkataba mpya kodi za fremu uliosainiwa kati ya manispaa na wafanyabiashara ndio kiwango walichokubaliana walipe.

No comments