Ads

Viongozi wa Umoja wa Vijana Kanisa la Mennonite Tanzania watakiwa kuongoza kwa kuzingatia misingi na vipaumbele vya kanisa

Viongozi wa  Umoja wa Vijana wa Kanisa la Mennonite Tanzania (KMT)wametakiwa kuongoza waumini wao kwa kuzingatia misingi, imani na vipaumbele vya kanisa hilo ikiwemo  Uinjilisti na kuieneza,Katiba,Sera, Kanuni na mifumo ya uongozi na utawala bora, na  pamoja huduma za maendeleo  na Ustawi jamii.
Aidha viongozi hao wamekumbushwa kuyawasilisha maono yao mbele ya kanisa hilo ili yaweze kufanyiwa kazi na kuratibiwa kwa manufaa ya kanisa.
Hayo yalisemwa mwishoni wa wiki na Askofu wa Kanisa hilo- Dayosisi ya Mashariki, Nelson Kisare katika Semina ya Uongozi wa Vijana iliyoandaliwa na umoja huo- Dayosisi ya Mashariki.
Alisema kanisa hilo hilo linatambua mchango wa vijana ndio maana lina viongozi wanaotoka umoja wa vijana wanaochaguliwa kwa demokrasia hivyo hawatakiwi kuogopa wala kuyaficha maono yao bali wawashirikishe wenzao kisha kuyawasilisha kanisani yafanyiwe kazi.
“ Viongozi wanapaswa kuongoza kwa kuzingatia imani na misingi bila ya kufanya hivyo kanisa haliwezi kusonga hata migogoro hutokea sababu ya kutokuwa na mwelekeo mmoja,” alisema Askofu Kisare.
Alibainisha kuwa viongozi wa KMT hawatakiwi kuwa wanafiki na wabinafsi wanatakiwa kusimamia ukweli na kutoa maamuzi ya haki ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea ndani ya kanisa.
Aliwasisitiza viongozi hao kutenga muda vizuri  katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo kujadili mipango na mikakati ya kuleta mabadiliko na maendeleo ya kanisa hilo.
Kwa upande wake, Katibu wa Taifa wa Kanisa hilo, Mchungaji John Wambura alisema wana malengo kuwafikia watu wapya milioni moja katika miaka 15 ijayo kwa kuhakikisha kila mwaka wanawafikia watu 70,000 pamoja kujenga makanisa 350 yenye uwezo uwezo wa kuingiza waumini 200 na kuzalisha watumishi 350 kila mwaka.
Mchungaji Wambura alisema kanisa hilo lina malengo ya kumiliki angalau chuo kikuu kimoja chenye Vitivyo vya Theolojia, Afya ,Elimu na Biasharahuku akibainisha dhamira ya KMT kuhubiri injili ya Yesu Kristu iletayo uwokovu, upendo, msamaha, haki na amani.
Kwa upande wake Mwalimu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Simon Laizer aliwasihi kutekeleza majukumu yao kikamilifu bila kujali kuyumbishwa na watu wasiowatakia mema wao na kanisa.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Kanisa hilo- Dayosisi ya Mashariki Mourice Mbunde alisema majimbo yaliyoshiriki ni Upanga, Ukonga, Tanga, Nyantira, Sinza, Segerea, Kusini, Kisota, Morogoro, Mikese na Temeke.
Aliwahimiza viongozi wa umoja kuhakikisha kabla hawajapanga mipango mikakati ya majimbo yao kuwashirikisha wanachama wenzao ili kupata mawazo yatayojenga kanisa imara.

No comments