Upatikanaji wa Mbolea Nchini sasa ni Zaidi ya Asilimia 82.
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Mamlaka ya udhibiti wa mbolea Tanzania (TFRA) imewahakikishia
wakulima kuwa upatikanaji wa mbolea hapa nchini ni wa uhakika na wakulima
wasiwe na hofu katika kipindi hiki ambacho msimu wa kilimo wa mwaka
2018/2019 unatarajia kuanza.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam leo, Kaimu Mkurugezi
Mtendaji wa Mamlaka hiyo Lazaro Kitandu alisema kuwa
kwa sasa kuna zaidi ya asilimia 82 ya mbolea inayopatikana nchini katika
kipindi cha mwanzo wa msimu wa kilimo, hali ambayo itasaidia wakulima
kufanya shughuli zao bila wasiwasi.
“Kwa sasa tayari tuna zaidi ya asilimia 82 ya mbolea
katika kipindi hiki cha mwanzo wa msimu, na kiasi kingine kilichobaki
tunaweza kuagiza kwa sababu muda tunao wa kutosha, na hivyo wakulima
wanaweza kuendelea na shuguli za kilimo bila kuhofia upatikanaji wa
mbolea “ alisema.
Alifafanua kuwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2018/2019,
makisio ya mahitaji ya mbolea kwa nchi nzima yatakuwa tani 514,138,
ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 14 ikilinganishwa na matumizi
ya mbolea katika msimu wa kilimo wa mwaka 2017/2018 ambapo mbolea ilikuwa
tani 450,000, aidha, hadi kufikia mwezi Novemba 8 mwaka huu jumla
ya tani 422,088 za mbolea zilikuwepo nchini, ikiwa ni ni takribani asilimia
82 yamahitaji ya mbolea kwa msimu wa kilimo kwa mwaka 2018/2019.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi huyo alisema kuwa,kutokana
na mfumo wa sasa wa Serikali ambao unadhibiti uingizaji na usambazaji
wa mbolea nchini umesaidia kuwa na kiasi hicho kikubwa cha mbolea
kwa mwaka huu.
Aliongeza kuwa, katika msimu wa kilimo wa mwaka
2017/2018 mahitaji ya mbolea za kupandia yaani (DAP) zilizoingizwa
kwa mfumo wa ununuzi wambolea kwa pamoja (BPS) zilikuwa tani 80,859.
Ambapo hadi kufikia Novemba 7 mwaka huu tayari kulikuwa na jumla
ya tani 95,712 za mbolea aina ya DAP hapa nchini, ikiwa ni zaidi ya
asilimia 100 ya mahitaji ya mbolea kwa msimu mzima.
Halikadhalika, mbolea inayotengenezwa hapa nchini
katika kiwanda cha Minjingu ambayo inatumika kwa ajili ya kupandia na
kukuzia mazao tayari imeshasambazwa katika mikoa mbalimbali kiasi cha
tani 6,548 .
Upatikanaji wa mbolea nchini umechangiwa kwa kiasi
kikubwa na sera wezeshi zilizowekwa na Serikali ikiwa ni pamoja na Mfumo
wa Uigizaji wa Mbolea kwa pamoja yaani BPS kwa lengo la kuwa na uhakika
wa upatikanaji wa mbolea hapa nchini pamoja na punguzo la bei kwa mkulima.
Mamlaka ya udhibiti wa mbolea (TFRA) ni taasisi ya
Serikali chini ya Wizara ya Kilimo ambayo ina jukumu la kusimamia na
kudhibiti utengenezaji,uingizaji na uuzaji wa mbolea hapa nchini.
Post a Comment