Ads

SIKONGE YAPATA BENDERA NYEUSI KWA KUSHIKA MKIA KATIKA MITIHANI MBALIMBALI MKOANI TABORA.

NA TIGANYA VINCENT-RS TABORA
HALMASHAURI ya Wilaya ya Sikonge imepata bendera nyeusi baada ya kwa kufanya vibaya na kuwa ya mwisho mkoani Tabora katika matokeo ya mitihani ya ngazi mbalimbali ya elimu.
Bendera hiyo imekabidhiwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri kwa  Uongozi wa Sikonge wakati wa kikao cha wadau wa elimu kilichokuwa kikiangalia hali ya elimu mkoani humo.
Aliwataka Sikonge kujiuliza kwanini wao ndio katika Mkoa mzima wamefanya vibaya katika mitihani ya kumaliza elimu ya Msingi, Kidato cha Nne na ile ya kujipima ya Darasa la Nne.
Mwanri alisema ni jukumu lao la kuhakikisha wanafanya kazi kwa nguvu ili kusahihisha makosa yao na hatimaye matokeo ya mitihani ijayo waweze kuikabidhi bendera hiyo kwa Halmashauri nyingine wakitoka mkiani.
Akizungumza kabla ya kupokea bendera Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Upendo Nganda alisema kufanya vibaya huko kumesababishwa na mpasuko uliopo Sikonge ambao umesababisha kutokuwepo na nidhamu miongoni mwa watumishi na viongozi.
Alisema baadhi ya watumishi wa ngazi ya chini hawaheshimu hata viongozi jambo ambalo limesababisha kutokuwepo umoja ambao ndio ungewasaidia kufanya vizuri katika nyanja mbalimbali.
Nganda aliomba uongozi wa Mkoa usaidie kuingilia kati mgogoro huo ili Halmashauri hiyo iweze kufanya vizuri katika maeneo mbalimbali.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Tabora Hassan Wakasubi aliahidi kuwachukulia hatua wale wote ambao wanachochea mgogoro huo ili kutafuta ufumbuzi wa tatizo ambalo linalosababisha mpasuko na kufanya Halmashauri hiyo ilifanye vizuri katika mitihani mbalimbali.
Alisema hata kama ni Mwanasiasa au Madiwani watamshughulikia kwa mujibu wa taratibu na Katiba ya CCM na kutafuta mgogoro unamnufaishaje mhusika  ili hatimaye wamchukuliea hatua kwa ajili ya kurejesha ushirikiano.
Wakasubi aliongeza kama ni mtumishi ndio chanzo cha mgogoro huo atashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma na kama ni wale wa kuteuliwa atamweleza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili amchukulie hatua.
Alisema kuwa haiwezekani wananchi wakashindwa kuendelea kwa sababu ya kukosa msaada kwa wataalamu kwa sababu ya migogoro inatengenezwa kwa maslahi binafsi.
Halmashauri ya Sikonge imekuwa ya mwisho katika Matokeo ya kumaliza elimu ya msingi, Kidato cha Nne na mtihani wa kujipima wa Darasa la Nne.

No comments