Ads

MRADI WA NG’OMBE KUWANUFAISHA WANAWAKE WA VIJIJINI WILAYANI NGORONGORO

  Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Hashim Mgandilwa akiongea na wakazi wa Ngorongoro wakati wa kukabidhi Ng’ombe hao 
 Robert Kamakia kutoka shirika la PALISEP akimkabidhi Mkuu wa Wilaya Mhe. Hashim Mgandilwa risala kuhusu makabidhiano hayo. 
Theresia Irafay, Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Ngorongoro akizungumza wakati wa ugawaji wa Ng’ombe hao.
 Laurent Wambura kutoka shirika la Oxfam akizungumza wakati wa ugawaji wa Ng’ombe hao.
Mh. Hashim Mgandilwa, Mkuu wa wa Wilaya ya Ngorongoro akikabidhi Ng’ombe kwa wanawake wa wilaya ya Ngorongoro.
 Wakazi wa vijiji vya Enguserosambu, Naan, Ng’arwa na Orkiu Juu wakihudhuria ugawaji wa Ng’ombe uliofanyika katika kijiji cha Enguserosambu.
 Picha ya pamoja 
……………………………………………………………………………………………………..
Wanawaken wenye kipato cha chini kutoka vijiji vinne vya wilaya ya
Ngorongoro wamekabidhiwa Ng’ombe ili kuwasaidia kuondokana na umasikini.

Wanawake hao wapatao 28 kutoka vijiji vya Enguserosambu, Naan, Ng’arwa na Orkiu
Juu walichaguliwa kulingana na hali yao ngumu ya maisha inayowapelekea
wakati mwingine kunyanyaswa kijinsia kupitia mfumo dume. Wanawake
wengine 15 watakabidhiwa Ng’ombe wao mnamo mwezi Machi mwaka huu kufanya
idadi ya wanufaika kufikia 43.
Makabidhiano
hayo yaliyofanyika katika kijiji cha Enguserosambu yalihudhuriwa na
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, viongozi mbalimbali wa vijiji, pamoja na
wakazi wa eneo hilo.
Akikabidhi Ng’ombe hao Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Hashim Mgandilwa
aliwataka wanawake hao kuhifadhi vizuri mifugo hiyo ili iwasaidie
kujikwamua kiuchumi kwa kuuza bidhaa zitokanazo na Ng’ombe ikiwemo
maziwa. Aidha Mkuu huyo wa wilaya alitoa rai kwa viongozi wa vijiji
hivyo kuhakikisha kwamba inapotokea misaada kama hii iwanufaishe
walengwa ambao mara nyingi ni watu maskini ili kuwaepusha na balaa la
njaa.
Ng’ombe hao wametolewa kama msaada na shirika la Oxfam kupitia wadau wake shirika la PALISEP.
Akizungumza katika hafla hiyo Meneja wa programu ya wafugaji wa Shirika la Oxfam
ndugu Laurent Wambura alisema shirika lake limefanya hivi ili kuwainua
kiuchumi wanawake wenye kipato cha chini na kubadilisha mtazamo wa jamii
ione kwamba hata wanawake wanaweza kumiliki mali ikiwemo mifugo na
kubadilisha kabisa maisha yao.
Naye Mkurugenzi wa shirika la PALISEP Robert Kamakia alisema lengo la mradi
huo ni kuwezesha upatikanaji wa lishe bora na maziwa kwa familia zisizo
na uwezo pamoja na kupunguza makali ya magonjwa kwa watoto kama vile
utapiamlo. 
Hii sio mara ya kwanza kwa shirika la Oxfam kugawa Ng’ombe katika wilaya ya
Ngorongoro, mnamo mwaka 2014 wanawake wapatao 66 walinufaika na mradi
huu kwa kugawiwa ngo’mbe mmoja jike kila mmoja huku viongozi wa vijiji
vinne vya Enguserosambu, Naan, Ng’arwa na Orkiu Juu wakikabidhiwa madume
6 wa mbegu kama sehemu ya kuboresha mifugo ili kukidhi mahitaji ya
soko. Ndama wote wanaozaliwa kama uzao wa kwanza wa Ng’ombe hawa
hugawiwa kwa wanawake wengine wenye kipato cha chini hivyo kunufaisha
jamii kubwa.

No comments