Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa amesema Serikali imepanga kufungua viwanda vya kusindika ngozi kwenye
mikoa ya Shinyanga, Geita na Dar es Salaam ili kutoa soko kwa ngozi za wanyama
wanaochinjwa kwenye machinjio ya mikoa hiyo.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Januari 18, 2016) wakati akizungumza na baadhi ya Watanzania waishio Botswana kwenye kikao kilichofanyika kwenye kituo cha mikutano ya kimataifa (GICC), jijini Gaborone, Botswana.
Waziri Mkuu alikuwa nchini Botswana kwa ziara ya siku moja
kumwakilisha Rais Dk. John Pombe Magufuli kwenye mkutano wa SADC Double Troika
yaani kikao maalum cha Wakuu wa Nchi na Serikali (SADC Summit) na Wakuu wa Nchi
wanaounda Chombo cha Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC Organ on
Politics, Defense and Security Cooperation) uliofanyika kwenye kituo cha
mikutano ya kimataifa (GICC), jijini Gaborone, Botswana.
Akizingumza na Watanzania hao, Waziri Mkuu alisema: “Tumeamua
kufungua viwanda vya kusindika ngozi kwenye mikoa ya Shinyanga, Geita na Dar es
Salaam (kule Pugu) ili ngozi zikishachunwa, zipelekwe moja kwa moja kiwandani,” alisema.
Alisema Serikali imeamua kuongeza viwanda nchini kama njia
mojawapo ya kukuza uchumi, kuacha kuuza mali ghafi lakini pia ni fursa ya
kuongeza ajira kwa Watanzania.
Akijibu hoja zilizoainishwa kwenye risala yao, Waziri Mkuu
alisema Serikali bado ina nia ya kuhamia Dodoma na kwamba itaendelea kutenga
fedha zaidi ili wizara nyingi zijenge ofisi zao Dodoma.
“Serikali ilikwishaamua kwamba Dodoma ni mji wa kiserikali na
Dar es Salaam ni mji wa kibiashara. Kwa sasa kuna baadhi ya Wizara zimeshajenga
ofisi Dodoma na kuna taasisi kama vile Benki Kuu nazo pia zimejenga ofisi zake
Dodoma. Tutaendelea kutenga fedha zaidi ili wizara nyingine zikamilishe ujenzi
wa ofisi zao,” alisema.
Waziri Mkuu Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania
waishio ughaibuni (Diaspora) watafute fedha za mitaji ama zao ama kupitia kwa
marafiki zao ili waweze kuwekeza nyumbani (Tanzania).
“Nia ya Serikali sasa hivi ni kufungua milango kwa wawekezaji
hasa wenye nia ya kujenga viwanda. Njooni nyumbani muone ni eneo gani mnaweza
kuwekeza, kama mna miradi huku fungueni matawi kule nyumbani. Serikali
inajivunia uwepo wenu kwa sababu inatambua kwamba huku mliko kuna kitu
mnajifunza na mnaweza kukirudisha nyumbani kwa manufaa ya Watanzania na Taifa
kwa ujumla,” alisema.
Mapema, akisoma risala yao kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa
Chama cha Watanzania waishio nchini Botswana (The Association of Tanzanians in
Botswana – ATB), Bw. Neiman Kissasi alisema chama hicho kilianzishwa mwaka 1992
kikiwa na lengo la kuwaunganisha Watanzania waishio Botswana pamoja kujenga
undugu wao na kusaidiana.
Katika risala yao, walishauri wafugaji wa Tanzania waelimishwe
na kuwezeshwa kufuga kisasa na kuondokana na ufugaji wa kurandaranda. Pia
waliiomba Serikali iongeze kasi ya mpango wake wa kuhamisha shughuli zote za
Serikali mjini Dodoma, kwani itasaidia kupunguza matumizi ya Serikali kwa kuwa
shughuli za Serikali zitakuwa zinafanyika eneo moja.
Vilevile, waliiomba Serikali ifungue fursa za kiuchumi kwenye
mikoa mingine ya Tanga, Lindi, Mtwara, Pwani, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Arusha
badala ya kuziacha ziwe Dar es Salaam peke yake. “Hii itasaidia kuibua fursa za
kiuchumi na kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam”, ilisema sehemu
ya risala yao.
Waziri Mkuu alirejea jijini Dar es Salaam jana usiku (Jumatatu,
Januari 18, 2016.)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,2 MTAA WA MAGOGONI,
S .L. P. 3021,11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, JANUARI 19, 2016
Post a Comment