BUNGE NA VIKAO VYAKAMATI KUANZA TAREHE 21 _25 JAN 2016
Ofisi ya Bunge inapenda kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge na
Wananchi kwa ujumla kuwa, uteuzi wa wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge
utafanyika kesho Alhamisi tarehe 21 Januari, 2016, na kufuatiwa na Uchaguzi wa
Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati husika pamoja na Kamati kupatiwa
maelezo juu ya Wajibu, kazi na Mipaka ya kazi ya Kamati na kupokea na kujadili
Mpango kazi wa Kamati unaoishia Juni, 2016.
Kwa kuzingatia Kanuni ya 111 ya Kanuni za kudumu za Bunge, Toleo
la Aprili, 2013 siku ya Ijumaa tarehe 22 hadi Jumamosi tarehe 23 Januari
kutakuwa na Mkutano wa Wabunge wote ambao pamoja na mambo mengine utakuwa na
lengo la kuwafahamisha Wabunge kuhusu Kanuni za Kudumu za Bunge na Uendeshaji
wa Bunge, Nadharia ya mgawanyo wa Madaraka katika Mihimili ya Dola, Haki, Kinga
na Madaraka ya Bunge na Mambo Mengine ya Kiserikali.
Aidha, Kikao cha kwanza cha Kamati ya Uongozi ambacho wajumbe
wake ni Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge chini ya Uenyekiti wa Mhe.
Spika, kinatarajiwa kufanyika Siku ya Jumapili tarehe 24 Januari, 2016, ambapo
Jumatatu tarehe 25 Januari, 2016 itakuwa ni siku mahususi kwa Wabunge kupata
maelezo kuhusu Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano unaokusudiwa kutekelezwa katika
Jamhuri ya Muungano.
Ratiba ya Shughuli za Mkutano wa pili wa Bunge unaotarajiwa
kuanza Jumanne tarehe 26 Januari, 2016 itatolewa baadae.
Imetolewa na,
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano.
Ofisi ya Bunge,
S.L.P 9133,
DAR ES SALAAM
20 Januari, 2016.
Post a Comment