Ads

DSE: MASOKO YA MITAJI NI FURSA YA UFADHILI WA MIRADI YA HALMASHAURI

 


DAR ES SALAAM: 

Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limehimiza Halmashauri nchini kutumia fursa zinazopatikana katika masoko ya mitaji kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Wito huo umetolewa katika warsha ya mafunzo kuhusu ufadhili mbadala kwa Halmashauri kupitia fursa za masoko ya mitaji, inayofanyika Oktoba 15 na 16, 2026.

Katika warsha hiyo, Mkurugenzi wa Usimamizi na Uchunguzi wa Soko wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Exaut Julius, amesema masoko ya mitaji yanaweza kuwa chanzo cha ziada cha fedha kwa Halmashauri zinazolenga kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, hususan katika sekta za maji, afya, usafi wa mazingira, masoko, vituo vya mabasi, majengo ya biashara na miundombinu mingine ya kiuchumi.

Amesema kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za kijamii na miundombinu kunahitaji Halmashauri kubuni njia mbadala na endelevu za kugharamia miradi ya maendeleo badala ya kutegemea chanzo kimoja cha fedha.

Kwa mujibu wa Bw. Julius, ingawa ruzuku za Serikali na mapato ya ndani vinaendelea kuwa vyanzo muhimu vya fedha kwa Halmashauri, masoko ya mitaji yanaweza kutoa fursa ya kuongeza rasilimali fedha kwa ajili ya miradi inayokidhi vigezo vinavyohitajika.


Ameeleza kuwa baadhi ya nyenzo zinazoweza kuchunguzwa ni pamoja na hati fungani za miundombinu, hati fungani za kijani na mifumo mingine ya ufadhili inayoruhusiwa kisheria, kulingana na aina ya mradi na uwezo wake wa kifedha.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa si kila mradi unafaa kufadhiliwa kupitia masoko ya mitaji, akibainisha umuhimu wa kufanya tathmini ya kina ya gharama, mapato yanayotarajiwa, vihatarishi na uwezo wa kutimiza wajibu wa kifedha kwa wawekezaji.

Akizungumzia usimamizi wa ufadhili kupitia masoko ya mitaji, Bw. Julius amesema upatikanaji wa fedha unapaswa kuambatana na uwazi, utawala bora, uwajibikaji na ulinzi wa wawekezaji


Amesema taasisi zinazotaka kutumia fursa hizo zinapaswa kuwa na mifumo madhubuti ya utoaji wa taarifa za kifedha, usimamizi wa vihatarishi na uzingatiaji wa sheria na kanuni zinazosimamia masoko ya mitaji.

Ameongeza kuwa maandalizi bora ya miradi ni muhimu katika kujenga imani ya wawekezaji na kuhakikisha fedha zitakazopatikana zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Bw. Julius amesema ushirikiano kati ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI, CMSA, DSE na Halmashauri ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inaandaliwa kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya ufadhili kupitia masoko ya mitaji.

Ameeleza kuwa TAMISEMI ina nafasi muhimu katika kuratibu mipango ya maendeleo ya Serikali za Mitaa, huku CMSA na DSE zikichangia katika maeneo yao ya kitaalamu ili kuwezesha Halmashauri kuelewa na kutumia fursa za masoko ya mitaji.

Aidha, amesema mifumo kama Special Purpose Vehicles (SPVs) inaweza kuchunguzwa kama mojawapo ya njia za kimuundo za kutekeleza miradi, kwa kuzingatia mahitaji ya mradi na masharti ya kisheria.

Katika warsha hiyo, washiriki wanatarajiwa kujengewa uwezo wa kutambua miradi inayoweza kufadhiliwa kupitia masoko ya mitaji, kuchagua nyenzo zinazofaa za ufadhili na kuelewa maandalizi yanayohitajika kabla ya kuwasilisha miradi kwa wawekezaji.

Masuala mengine yatakayojadiliwa ni pamoja na vyanzo vya mapato kwa ajili ya kutimiza wajibu wa kifedha, majukumu ya Halmashauri katika usimamizi wa miradi na taratibu zinazopaswa kufuatwa ili kukamilisha mchakato wa kupata ufadhili.

Washiriki wamehimizwa kutumia fursa hiyo kuuliza maswali, kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa mifumo ya ufadhili mbadala.

Matarajio ni kwamba mafunzo hayo yatasaidia Halmashauri kubaini miradi ya kipaumbele inayoweza kuandaliwa kwa ajili ya kutafuta ufadhili kupitia masoko ya mitaji.

Warsha hiyo ya siku mbili inalenga kuimarisha uelewa wa Halmashauri kuhusu fursa za masoko ya mitaji na namna zinavyoweza kuchangia katika kupanua wigo wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo nchini.



No comments