Ads

TANZANIA KUJENGA CHUO KIKUU CHA USAFIRI WA MAJI CHA KIKANDA

 


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

TANZANIA imechaguliwa kuwa nchi itakayojenga Chuo Kikuu cha Kikanda cha Usafiri kwa Njia ya Maji (Regional Maritime University – RMU), hatua inayolenga kuimarisha elimu, mafunzo, utafiti na ubunifu katika sekta ya usafiri wa majini kwa nchi wanachama wa Shirika la Bahari la Kanda ya Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini mwa Afrika (MOESNA).


Akizungumza Kwa na waandishi wa habari kwaniaba ya Waziri wa uchukuzi Naibu waziri wa Wizara ya uchukuzi Mhe.David Kihenzile , amesema chuo hicho kinatarajiwa kuwa kituo cha kikanda cha umahiri kitakachosaidia kukidhi mahitaji ya wataalamu wa usafiri wa majini, kuimarisha utafiti na ubunifu na kuandaa kizazi kipya cha wataalamu wa sekta hiyo.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 10 wa Baraza la Mawaziri wa MOESNA, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 15, 2026, katika Hoteli ya Johari Rotana, Kihenzile amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na shirika hilo pamoja na nchi wanachama katika hatua zinazofuata za utekelezaji wa mpango huo.


“Ndugu wanahabari, napenda kuwataarifu kuwa Chuo Kikuu cha Kikanda cha Usafiri kwa Njia ya Maji (Regional Maritime University – RMU) kitajengwa nchini Tanzania,” alisema Profesa Mbarawa.


Alisisitiza kauli hiyo kwa kurudia kwamba chuo hicho kitajengwa nchini Tanzania, akionesha umuhimu wa mradi huo katika kuendeleza sekta ya usafiri wa majini na kuimarisha uwezo wa nchi wanachama katika elimu na mafunzo ya kitaalamu.


Alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo tayari kushirikiana kikamilifu na MOESNA na nchi wanachama katika hatua zinazofuata ili kuhakikisha chuo hicho kinafikia malengo yaliyokusudiwa.


“Dhamira yetu ni kuona chuo hicho kikiwa kituo cha umahiri cha kikanda kinachohudumia mahitaji ya nchi zote wanachama, kuimarisha utafiti na ubunifu, na kujenga kizazi kipya cha wataalamu wa sekta ya usafiri kwa njia ya maji,” alisema.


Kihenzile amesema maendeleo ya sekta ya usafiri wa majini hayawezi kutegemea uwekezaji katika bandari, meli na miundombinu pekee, bali yanahitaji pia kuimarisha rasilimali watu kupitia elimu, mafunzo, utafiti, teknolojia na ubunifu.


Alieleza kuwa miundombinu bila ujuzi haiwezi kutoa manufaa yake kikamilifu, huku teknolojia bila wataalamu waliopata mafunzo stahiki ikishindwa kuleta matokeo endelevu.


Aidha, alisema mifumo ya udhibiti wa sekta hiyo inahitaji wataalamu wenye weledi ili kuhakikisha usalama na ulinzi wa usafiri wa majini vinazingatiwa kwa manufaa mapana ya taifa.


Kwa mujibu wa Waziri huyo, MOESNA imeendelea na mchakato wa kuanzisha chuo hicho ili kiwe kituo cha kikanda cha elimu, mafunzo, utafiti na ubunifu katika sekta ya usafiri wa majini.


Alisema hatua hiyo ina umuhimu katika kipindi ambacho nchi za Afrika zinaendelea kutekeleza Agenda 2063 yenye kaulimbiu ya “Afrika Tuitakayo” pamoja na Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), unaolenga kuondoa vikwazo vya biashara, kuongeza biashara baina ya nchi za Afrika na kukuza viwanda.


Alibainisha kuwa kufanikisha malengo hayo kunahitaji mifumo ya uchukuzi na lojistiki yenye ufanisi, ikiwemo bandari, meli, reli, barabara, njia za majini, vituo vya mizigo na teknolojia zinazounganisha mifumo hiyo.


Katika muktadha huo, chuo hicho kinatarajiwa kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha maarifa na ujuzi wa wataalamu watakaohitajika katika kuendeleza sekta ya usafiri wa majini na kuchangia ushindani wa Afrika katika biashara ya kikanda na kimataifa.


Mkutano Mkuu wa 10 wa Baraza la Mawaziri wa MOESNA unatarajiwa kujadili masuala mbalimbali yanayohusu uimarishaji wa biashara kwa nchi wanachama, ikiwemo nchi zisizo na bahari na zile zenye ukanda wa bahari.


Mkutano huo utahudhuriwa na takribani mawaziri 26 wanaoshughulikia masuala ya uchukuzi na lojistiki, pamoja na wawakilishi wa taasisi za kikanda na kimataifa zinazoshiriki katika maendeleo ya usafiri wa majini.


Tanzania ina nafasi ya kimkakati katika Bahari ya Hindi na maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa, hali inayoipa nafasi muhimu katika kuwezesha biashara kati ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini na masoko ya dunia.


Ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kikanda cha Usafiri kwa Njia ya Maji nchini Tanzania unaweka msingi wa ushirikiano wa kikanda katika elimu na mafunzo ya sekta hiyo, huku Serikali ikieleza utayari wake wa kushirikiana na MOESNA na nchi wanachama katika hatua zinazofuata za utekelezaji wa mradi huo.

No comments