NAIBU WAZIRI MKAMA :TEKNOLOJIA NI UFUNGUO WA MUSTAKABALI WA SEKTA YA POSTA
Dar Es Salaam – Serikali imewataka watoa huduma za posta na usafirishaji wa haraka nchini kuharakisha kujiunga na mifumo ya kidijitali ya ufuatiliaji wa nyaraka, vifurushi na vipeto ili kuwawezesha wateja kupata taarifa sahihi kuhusu mahali mizigo yao ilipo katika hatua zote za usafirishaji.
Wito huo umetolewa na Naibu waziri wizara ya mawasiliano, TEKNOLOJIA ya habari, Dkt Switbert Zacharia Mkama wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani yaliyofanyika leo oktoba 9, 2026, jijini Dar es Salaam, akisisitiza kuwa mifumo hiyo itaongeza uwazi, usalama na ufanisi katika sekta ya posta.
Mkama amesema baadhi ya wateja wamekuwa wakikosa taarifa za uhakika kuhusu safari za mizigo yao, hali inayoweza kupunguza imani katika huduma za usafirishaji. Ameeleza kuwa matumizi ya mfumo wa ufuatiliaji yatawezesha wateja kujua hatua mbalimbali za safari za mizigo yao kupitia taarifa zinazotumwa kwenye simu zao.
Amesisitiza kuwa Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Shirika la Posta Tanzania (TPC) inapaswa kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa watoa huduma ambao bado hawajaunganishwa na mfumo wa ufuatiliaji wa mizigo unaohusishwa na mfumo wa CMS wa TCRA.
“Lazima wafanye hivyo kwa haraka kwa sababu mteja anataka kujua mzigo wake uko wapi. Kama hujajiunga, maana yake mzigo wako unakwenda gizani,” amesema Mkama.
Ameongeza kuwa mfumo huo unaweza kuboresha hata huduma za usafirishaji wa mizigo kupitia mabasi, kwa kuwezesha wateja kufuatilia mizigo yao bila kutegemea mawasiliano ya moja kwa moja na wahudumu wa usafiri.
Aidha, Mkama amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya sekta ya posta kupitia uboreshaji wa sera, sheria, kanuni, miundombinu na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kukidhi mahitaji ya wananchi na wafanyabiashara.
Amesema sekta ya posta inakabiliwa na mabadiliko makubwa yanayotokana na ukuaji wa biashara mtandao na maendeleo ya teknolojia, hivyo kuna umuhimu wa kuhakikisha huduma zinazotolewa ni za haraka, salama, nafuu na zinazofikika kwa wananchi wote, wakiwemo waishio vijijini.
Katika hatua nyingine, amesisitiza umuhimu wa kukamilisha na kuboresha Mfumo wa Taifa wa Anwani za Makazi, akieleza kuwa mfumo huo ni msingi muhimu katika kurahisisha usafirishaji na ufikishaji wa nyaraka, vifurushi na vipeto pamoja na utoaji wa huduma nyingine za Serikali.
Akizungumzia kaulimbiu ya Siku ya Posta Duniani ya mwaka huu, “Mtandao mmoja wa posta, uwezeshaji usio na kikomo,” Mkama amesema ushirikiano wa wadau na matumizi ya teknolojia ni muhimu katika kuimarisha sekta hiyo, kukuza biashara za ndani na kimataifa, kuongeza fursa za ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Pia amewapongeza Shirika la Posta Tanzania na wadau wengine kwa kuandaa shindano la uandishi wa barua lililowapa vijana fursa ya kukuza ujuzi wa uandishi, lugha na ubunifu. Amepongeza pia watoa huduma za usafirishaji wa haraka walioanza kuunganisha mifumo yao na mfumo wa CMS wa TCRA.
Mkama amewataka wadau wa sekta ya posta kuendeleza uwekezaji katika teknolojia na miundombinu, kuimarisha usalama wa taarifa za wateja na kuhakikisha huduma bora za posta zinawafikia Watanzania wote.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kubaini changamoto na kuchukua hatua zinazolenga kuifanya sekta ya posta kuwa ya kisasa, shindani na yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.




Post a Comment