Ads

Angel Abayo na mtoto wa miezi 10 wapatikana salama Dar es Salaam

 

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetangaza kupatikana kwa Angel Abayo, mwenye umri wa miaka 19, ambaye ni mfanyakazi wa ndani aliyedaiwa kutoweka pamoja na mtoto wa mwajiri wake mwenye umri wa miezi 10 katika eneo la Kibada, Kigamboni.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Dar es Salaam ambaye pia ni Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Faustine Mafwele, imeeleza kuwa katika upelelezi wa awali, Angel alisema alilazimika kuondoka na mtoto huyo bila mwajiri wake kufahamu baada ya kuomba ruhusa ya kwenda Kibaha kumwona ndugu yake aliyekuwa akiugua, lakini ombi hilo likakataliwa.

Angel na mtoto huyo walipatikana wakiwa salama, kufuatia juhudi za ufuatiliaji zilizofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine wa masuala ya kiuchunguzi.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewashukuru wananchi na wadau wote walioshiriki katika ufuatiliaji na kuwezesha kupatikana kwa Angel na mtoto huyo salama.

Aidha, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kuhusu matukio ya uhalifu na masuala yanayohusu usalama, hatua inayosaidia kuimarisha amani na utulivu katika Jiji la Dar es Salaam.

Jeshi hilo pia limewaalika wananchi kushiriki katika kampeni ya “Ongea na Kamanda”, inayolenga kuwafikia wananchi katika maeneo yao, kusikiliza changamoto zinazohusiana na uhalifu na usalama, pamoja na kushirikiana kutafuta ufumbuzi.

No comments