Ads

Nsekela awataka wafanyakazi wa CRDB kwenda na wakati kuwahudumia wateja

 





DAR ES SALAAM: Mkurugenzi Mkuu wa CRDB Bank, Abdullmajid Nsekela, amewataka wafanyakazi wa benki hiyo kuongeza ubunifu na kwenda hatua ya ziada (extra mile) katika kuwahudumia wateja, akisisitiza umuhimu wa kuwasikiliza, kuchukua hatua kwa wakati na kuhakikisha wanapata suluhisho bila kuzungushwa.

Nsekela alitoa kauli hiyo wakati akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, ambapo alisisitiza kuwa kila mfanyakazi anapaswa kujiuliza iwapo amemsikiliza mteja, amechukua hatua gani kutatua changamoto yake na amefanya nini kurahisisha huduma kwake.

Alisema miongozo na taratibu za benki ni muhimu katika kuhakikisha huduma zinaendeshwa kwa viwango vinavyotakiwa, lakini hazipaswi kuwa kikwazo kwa mfanyakazi kutumia akili na ubunifu kumsaidia mteja.

“Tunatumia miongozo yetu. Miongozo ni standard, lakini haikuzuii kutumia akili ya ziada. Kutumia akili ya ziada ndiyo kutatufanya kwenda extra mile kwa mteja wetu,” alisema.

Nsekela alisema mteja hahitaji kufahamu muundo wa ndani wa benki, idara zinazohusika au nani anayewajibika katika kila hatua ya mchakato, bali anahitaji kusikilizwa na kupewa suluhisho kwa wakati.

Alisema kwa msingi huo, mfanyakazi hapaswi kumrudisha mteja kutoka idara moja kwenda nyingine kwa sababu huduma anayohitaji inahusisha kitengo tofauti, bali anapaswa kuchukua jukumu la kumsaidia kupata majibu au kumwelekeza kwa usahihi.

“Tunapaswa kujiweka katika nafasi ya mteja ili kuelewa changamoto anayopitia na kutafuta njia rahisi na yenye ufanisi ya kumsaidia,” alisema.

Maoni ya wateja ni fursa ya kuboresha huduma

Mkurugenzi huyo pia alisisitiza umuhimu wa kusikiliza maoni ya wateja, akisema mrejesho, ikiwemo malalamiko na maoni hasi, unapaswa kuchukuliwa kama fursa ya kuboresha huduma za benki.

“Comments zote ambazo siyo nzuri ni fursa kwetu kuboresha huduma zetu. Kutuandikia feedback haitusumbui, inatufanya kuwa bora zaidi,” alisema.

Alisema dhana ya extra mile haipaswi kuwa kampeni ya muda mfupi inayotekelezwa wakati wa wiki ya huduma kwa wateja pekee, bali inapaswa kujengwa kuwa sehemu ya utamaduni na tabia za wafanyakazi wa benki hiyo.

“Extra mile isiishie kwenye wiki hii. Tunataka iwe sehemu ya mabadiliko ya tabia zetu. Itakuwa imejengeka ndani ya utamaduni wetu. You must go extra mile,” alisema.

Viongozi watakiwa kuwa mfano

Nsekela aliwataka viongozi wa benki hiyo kuwa mfano katika utekelezaji wa dhana hiyo, huku kila mfanyakazi akitakiwa kutafuta namna ya kufanya zaidi ya kile kinachotarajiwa katika nafasi yake.

Alisema dhana hiyo pia inapaswa kuwahusisha wataalamu wa teknolojia na idara nyingine katika kubuni huduma na mifumo inayorahisisha maisha ya wateja.

Kwa mujibu wa Nsekela, huduma za benki ni mnyororo unaohusisha watu na idara mbalimbali, hivyo kila hatua inayochukuliwa na mfanyakazi ina mchango katika uzoefu wa mwisho wa mteja.

“Huduma ni mnyororo. Kuna watu wengi kwenye mchakato. Tunapaswa kuunganisha mnyororo huo katika kila hatua, kwa sababu mwisho wa siku tunamhudumia mteja,” alisema.

Apongeza wafanyakazi wa mstari wa mbele

Katika hatua nyingine, Nsekela aliwapongeza wafanyakazi wa mstari wa mbele, hususan wanaohudumia wateja moja kwa moja, kwa kazi wanayoifanya na kuwataka kuongeza juhudi zaidi katika kuwahudumia wateja.

“Naishukuru sana front office staff kwa kazi nzuri mnayoifanya. Kazi yenu imekuwa nzuri siku zote, lakini sasa ni wakati wa kwenda extra mile,” alisema.

Kwa upande wa wateja, Nsekela alisema CRDB Bank inawashukuru kwa kuendelea kuiamini na ina dhamira ya kulipa imani hiyo kwa kutoa suluhisho linalokidhi mahitaji yao, ushauri bora wa kifedha na kuwasaidia katika changamoto zao.

“Tungependa kulipa imani hiyo kwa kutoa solution ya mahitaji yenu. Tungependa kulipa imani hiyo kwa kuwa washauri bora katika mipango yenu ya uchumi na kubeba mzigo wa changamoto zenu ili tuweze kutafuta solution,” alisema.

No comments