Victory Financial yafungua milango ya uwekezaji kwa Sh10,000
DAR ES SALAAM
Watanzania wenye mitaji midogo sasa wamepata fursa ya kushiriki katika uwekezaji wa masoko ya mitaji kupitia mifuko miwili mipya ya uwekezaji wa pamoja iliyoanzishwa na Victory Financial Services Limited.
Mifuko hiyo ambayo ni Thamani Fund na Ushindi Fund, inalenga kuwafikia wawekezaji wenye viwango tofauti vya kipato na uwezo wa kuvumilia hatari, huku kiwango cha kuanzia kuwekeza kikiwa Sh10,000.
Akizungumza kuhusu mifuko hiyo, Mkurugenzi wa Biashara na Masoko wa Victory Financial Services, Amedeus Raphael Dogati, amesema uzinduzi huo ni sehemu ya jitihada za kampuni kupanua ushiriki wa Watanzania katika masoko ya mitaji na kuwapa fursa ya kuanza kujenga uwekezaji hata kwa kutumia kiasi kidogo cha fedha.
Amesema kampuni hiyo imekuwa ikifanya kazi katika sekta ya masoko ya mitaji tangu mwaka 2016, ikitoa huduma za udalali, ushauri wa uwekezaji na kuwawezesha wateja kushiriki katika ununuzi na uuzaji wa hisa pamoja na hati fungani.
Dogati amesema Ushindi Fund umeundwa zaidi kwa ajili ya wawekezaji wanaotanguliza uhifadhi wa mtaji, huku wakilenga kupata fursa ya kukuza fedha zao kwa muda.
Amesema takribani asilimia 80 ya mfuko huo itawekezwa katika hati fungani za Serikali na za taasisi, huku asilimia 20 iliyobaki ikiwekezwa katika hisa na masoko ya fedha.
Kwa kuanzia Sh10,000, amesema mfuko huo unalenga kuwawezesha watu wengi zaidi kuanza safari ya uwekezaji bila kuhitaji mtaji mkubwa.
Kwa kuzingatia muundo wake wa uwekezaji, Ushindi Fund una kiwango cha hatari cha chini hadi cha kati (low to medium).
Kwa upande mwingine, Thamani Fund umejikita zaidi katika soko la hisa na unalenga wawekezaji wanaotafuta fursa kubwa zaidi ya ukuaji wa mtaji kwa muda mrefu.
Dogati amesema takribani asilimia 70 ya mfuko huo itawekezwa katika hisa zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), wakati asilimia 30 ikiwekezwa katika hati fungani na masoko ya fedha.
Mwekezaji anaweza kuanza na Sh10,000, huku akiruhusiwa kuongeza uwekezaji wake kwa kiasi cha kuanzia Sh5,000.
Amesema mfumo huo unampa mwekezaji fursa ya kuwa na uwekezaji uliosambazwa katika kampuni mbalimbali, badala ya kutegemea hisa ya kampuni moja pekee.
“Uwekezaji wowote una hatari. Ndiyo maana usimamizi wa mifuko hii unafanywa na wataalamu wenye weledi na uzoefu katika sekta ya fedha,” amesema Dogati.
Kwa sababu sehemu kubwa ya fedha zake itaelekezwa katika hisa, Thamani Fund ina kiwango cha hatari cha kati hadi juu (medium to high).
Dogati amesema tofauti ya mifuko hiyo inamwezesha mwekezaji kuchagua bidhaa inayolingana na malengo yake ya kifedha, muda anaotarajia kuwekeza na kiwango cha hatari anachoweza kuvumilia.
Amesisitiza umuhimu wa wawekezaji kupata elimu na ushauri wa kitaalamu kabla ya kufanya maamuzi, badala ya kuwekeza bila kuelewa hatari na fursa zinazohusishwa na bidhaa wanayochagua.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, wawekezaji wanaweza kutumia majukwaa ya kidijitali, yakiwemo DSE Hisa Kiganjani na WebOTC, pamoja na tovuti ya Victory Financial Services.
Ofa ya awali ya uwekezaji katika mifuko hiyo ilianza Agosti 24, 2026 na inatarajiwa kufungwa Oktoba 22, 2026.
Uzinduzi wa mifuko hiyo unaifanya sekta ya uwekezaji kuwa rahisi kufikiwa na kundi pana zaidi la Watanzania, hususan wale ambao awali waliona uwekezaji katika masoko ya mitaji unahitaji mtaji mkubwa.


Post a Comment