HII NI AJALI MBAYA SANA KUWAHI KUTOKEA HAPA BUNJU
Dar es Salaam - Watu wanne wamefariki dunia baada ya basi la kampuni ya Abood kugongana na gari dogo aina ya Toyota IST katika eneo la Bunju Sokoni, Barabara ya Bagamoyo, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, ajali hiyo ilitokea Septemba 7, 2026 majira ya saa 1:40 usiku, baada ya basi lenye namba za usajili T 235 EMJ, aina ya Yutong, kugongana na gari lenye namba T 274 ERU, aina ya Toyota IST.
Basi hilo lilikuwa likitokea Tegeta kuelekea Bunju kwa safari ya kwenda mkoani Tanga, likiendeshwa na Christivian Steven Shemuhilu, mwenye umri wa miaka 38, mkazi wa Kange, Tanga.
Gari dogo aina ya Toyota IST lilikuwa likiendeshwa na Hamad Mohamed Juma maarufu Majid, mwenye umri wa miaka 37, mkazi wa Mtoni Mtongani, Dar es Salaam, ambaye ni miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo.
Wengine waliofariki ni Edward Kimanyara, mstaafu na mkazi wa Yombo Dovya, Temeke; Magdalena Manyenga, mwenye umri wa miaka 45, mkazi wa Temeke; na Melina Emmanuel Kayoka, mwenye umri wa miaka 42, mkazi wa Yombo Kisiwani, Temeke.
Jeshi la Polisi limetaja uzembe wa dereva wa basi katika kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara kuwa chanzo cha ajali hiyo.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala, Kinondoni, huku dereva wa basi hilo akishikiliwa na Polisi kwa hatua zaidi za kisheria.
Jeshi la Polisi limewataka watumiaji wote wa barabara, hususan madereva wa vyombo vya moto, kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani ili kuzuia ajali.

Post a Comment