Tanzania, Vietnam Kuimarisha Ushirikiano wa Kilimo na Biashara
Na. Hashim Mushi
DAR ES SALAAM: Tanzania na Vietnam zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika kilimo, uvuvi, ufugaji, biashara na uwekezaji, kufuatia mazungumzo ya siku mbili yaliyofanyika kati ya nchi hizo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Millya, amesema Tanzania na Vietnam zina uhusiano wa kidiplomasia tangu mwaka 1965, na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha uhusiano huo kwa manufaa ya wananchi.
Amesema Vietnam ina uzoefu mkubwa katika kilimo, hususan kilimo cha mpunga, na iko tayari kushirikiana na Tanzania katika teknolojia, ujuzi na mafunzo kwa wataalamu wa kilimo, ikiwemo kupitia Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA).
Mhe. Millya amesema mazungumzo hayo yamezaa matokeo baada ya kampuni za Tanzania, ikiwemo Mohammed Enterprises na Grow Cashon, kusaini mikataba na kampuni za Vietnam yenye thamani ya takribani Sh bilioni 800.
Amesema mikataba hiyo inatarajiwa kuongeza ajira, mapato ya Serikali kupitia kodi na upatikanaji wa fedha za kigeni.
Aidha, amesema Vietnam ni soko muhimu la korosho za Tanzania, huku akieleza kuwa takribani asilimia 70 ya mauzo ya korosho za Tanzania nje ya nchi yanafanyika na Vietnam.
Mhe. Millya pia ametaja uwekezaji wa Vietnam katika sekta ya mawasiliano kupitia kampuni ya Halotel, akisema umechangia kuwaunganisha wananchi wa vijijini, hususan wakulima, wafugaji na wavuvi, na masoko.
Ametoa wito kwa sekta binafsi na Watanzania kutumia fursa zinazotokana na kuimarika kwa uhusiano huo, akisisitiza kuwa Serikali imeweka mazingira ya kuwezesha biashara na uwekezaji.
“Sasa ni sekta binafsi kukimbilia fursa hizi, sio kusubiri Serikali ikuletee mlangoni mwako. Hizi ndio ajira na hii ndio kubadilisha maisha ya Watanzania,” amesema Mhe. Millya.

Post a Comment