Tanzania yaongoza mjadala wa mitaala inayozingatia utamaduni wa Afrika
DAR ES SALAAM: Tanzania imeendelea kushirikiana na nchi nyingine za Afrika katika kuandaa mitaala inayozingatia historia, utamaduni, mila na desturi za Afrika, huku ikilenga kumjenga Mwafrika mwenye uzalendo, maadili na fahari ya asili yake.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Anneth Komba, katika mkutano wa siku nne wa African Curriculum Association Conference, unaowakutanisha wadau na taasisi za mitaala kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Komba amesema kongamano hilo, ambalo ni la sita kufanyika, limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Tanzania na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania na Taasisi ya Elimu Zanzibar.
Amesema moja ya ajenda kubwa ya kongamano hilo ni kuhakikisha Afrika inaandaa mitaala inayozingatia uhalisia wa bara hilo, badala ya kuendelea kutegemea mifumo ya mitaala iliyoasisiwa kwa kiasi kikubwa na nchi zilizowahi kulitawala bara la Afrika.
“Kama bara tunayo ajenda ya kuhakikisha kwamba tunaandaa mitaala ambayo inazingatia uafrika wetu. Tukizingatia historia, kwa kiasi kikubwa tulikuwa tumecopy mitaala ya wenzetu waliotutawala,” amesema Komba.
Kwa mujibu wa Komba, lengo ni kuwa na mitaala inayomwandaa Mwafrika mzalendo, anayejivunia utambulisho wake, huku akiwa na maadili na uelewa wa mila na desturi za Kiafrika.
Amesema kwa siku tatu za mwanzo za kongamano hilo, washiriki watajadili masuala mbalimbali yanayohusu mitaala, huku siku ya nne ikiwa imetengwa kwa ajili ya ziara ya kutembelea shule nchini Tanzania.
Ameeleza kuwa ziara hiyo itawapa wageni fursa ya kuona utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa nchini na hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuimarisha elimu inayolenga kujenga maarifa na ujuzi kwa wanafunzi.
Komba amesema wanatarajia kongamano hilo kuzaa mambo makuu matatu, ambayo ni Azimio la Dar es Salaam kuhusu mitaala ya Afrika, mwongozo wa uandaaji wa mitaala barani Afrika, pamoja na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha uandaaji na utekelezaji wa mitaala katika nchi za Afrika.
Amesema mkutano huo ni sehemu ya jitihada za nchi za Afrika kujenga mifumo ya elimu inayokidhi mahitaji ya bara na kuandaa kizazi chenye ujuzi, maadili na utambulisho wa Kiafrika.

Post a Comment