Tanzania, Vietnam Kuimarisha Ushirikiano katika Maeneo ya Kimkakati
Dar es Salaam: Tanzania na Vietnam zimeeleza dhamira ya kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kisiasa na kidiplomasia, biashara na uwekezaji, kilimo na uvuvi, pamoja na sayansi na teknolojia.
Akizungumza kuhusu kikao cha serikali kati ya Tanzania na Vietnam, Mkurugenzi wa Idara ya Asia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Felista Rugambwa, amesema pande hizo zinajadili namna ya kuweka mifumo imara ya kisiasa, kidiplomasia na kisheria itakayosaidia kuimarisha na kukuza uhusiano wa nchi hizo.
Amesema eneo la pili ni biashara, uwekezaji na masuala ya fedha, ambapo Tanzania inalenga kuongeza idadi na aina ya bidhaa zinazouzwa katika soko la Vietnam.
Kwa mujibu wa Rugambwa, Vietnam ni miongoni mwa nchi zinazoagiza bidhaa kutoka Tanzania, zikiwemo korosho, pamba na kahawa, hivyo Serikali inaangalia namna ya kupanua wigo wa bidhaa zinazoweza kuingia katika soko hilo.
“Tunajua Vietnam ni miongoni mwa nchi ambazo zinaagiza bidhaa kutoka Tanzania, ikiwemo korosho, pamba, kahawa na bidhaa nyingine. Kwa hiyo tunaweka mifumo ya namna gani ya kuongeza idadi ya bidhaa zinazotoka Tanzania kwenda Vietnam,” amesema Rugambwa.
Amesema eneo lingine litakalojadiliwa ni kilimo, uvuvi na misitu, akibainisha kuwa Vietnam imepiga hatua katika sekta ya kilimo na Tanzania inalenga kutumia fursa hiyo kuimarisha ushirikiano wa sekta hiyo.
Amesema Tanzania inatarajia kuona wawekezaji kutoka Vietnam wakija kuwekeza katika kilimo nchini, ikiwemo kuendeleza mashamba na kuzalisha mazao kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Rugambwa, uwekezaji huo pia unatarajiwa kuchangia katika uanzishaji wa ajira na kuongeza fursa za kiuchumi kwa Watanzania.
Aidha, amesema pande hizo zinatarajia kuimarisha ushirikiano katika sayansi na teknolojia, ikiwemo kuongeza fursa za elimu na mafunzo kwa Watanzania pamoja na kuvutia uwekezaji zaidi kutoka Vietnam katika sekta hiyo.
“Tunafahamu kuwa kuna kampuni ya Vietnam inayofanya kazi hapa nchini na tunatarajia kuongeza ushirikiano, kutoa fursa za masomo kwa Watanzania, lakini pia kuwekeza zaidi katika eneo la sayansi na teknolojia hapa nchini,” amesema.
Amesema ushirikiano huo unalenga kuweka msingi mpana zaidi wa mahusiano kati ya Tanzania na Vietnam, kupitia kuimarisha diplomasia, biashara na uwekezaji, sekta za uzalishaji pamoja na uhamishaji wa maarifa na teknolojia.

Post a Comment