Ads

Tanzania na Vietnam Kuimarisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Biashara




Dar es Salaam. Tanzania na Vietnam zimeendelea kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara, huku Serikali ikieleza kuwa ushirikiano huo utawezesha Tanzania kujifunza uzoefu wa Vietnam katika maendeleo ya viwanda na kuongeza fursa za biashara kwa sekta binafsi.

Akizungumza kuhusu kikao cha pili cha Tume ya Pamoja ya Kiserikali (Joint Intergovernmental Commission) kati ya Tanzania na Vietnam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samwel Shelukindo, alisema kikao hicho ni muhimu kwa kuwa kinarejesha na kuimarisha majadiliano ya ushirikiano kati ya nchi hizo baada ya kikao cha kwanza kufanyika mwaka 2014.

Balozi Shelukindo alisema Vietnam ni miongoni mwa nchi ambazo zimepata maendeleo makubwa kiuchumi, hususan katika sekta ya viwanda, hivyo Tanzania inaweza kunufaika kwa kujifunza namna nchi hiyo ilivyofanikiwa kujenga mazingira ya uzalishaji na kuvutia viwanda.

“Uhusiano huu ambao tunauimarisha utatusaidia sana sisi Tanzania kujifunza kutoka kwa wenzetu wa Vietnam, hasa namna walivyofanikiwa kuwa na viwanda vingi,” alisema.

Alisema Vietnam pia ni soko muhimu kwa bidhaa za kilimo kutoka Tanzania, akitaja korosho na pamba miongoni mwa bidhaa zinazoweza kuimarisha zaidi biashara kati ya nchi hizo mbili.

Kwa mujibu wa Balozi Shelukindo, kikao hicho kinahusisha sekta mbalimbali, jambo analoeleza kuwa ni fursa kwa Tanzania na Vietnam kupanua maeneo ya ushirikiano na kuongeza manufaa ya kiuchumi kwa mataifa hayo.

Aidha, alisema ujumbe wa Vietnam umeambatana na wawakilishi wa sekta binafsi ambao wamekuwa wakitembelea maeneo mbalimbali nchini Tanzania kwa lengo la kutafuta fursa za uwekezaji na ushirikiano wa kibiashara.

“Ni fursa kubwa kwa sekta binafsi yetu kujaribu kushirikiana na sekta binafsi ya Vietnam kwa ajili ya kukuza biashara na kukuza uchumi wa nchi zetu mbili,” alisema.

Balozi Shelukindo alisisitiza kuwa kilimo, sayansi na teknolojia ni miongoni mwa maeneo muhimu ambayo Tanzania na Vietnam zinatarajia kuendelea kushirikiana.

Alisema kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, hivyo uzoefu na teknolojia kutoka Vietnam vinaweza kusaidia kuongeza uzalishaji, thamani ya mazao na fursa za biashara.

Katika eneo la sayansi na teknolojia, alitaja uwepo wa kampuni za Vietnam nchini Tanzania, ikiwemo Halotel, kama mfano wa ushirikiano ambao umechangia katika kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kiteknolojia kati ya nchi hizo.

Balozi Shelukindo alisema Tanzania inalenga kutumia ushirikiano huo katika sekta hizo mbili pamoja na maeneo mengine yenye maslahi ya pamoja, ili kuongeza biashara, uwekezaji na kukuza uchumi wa nchi zote mbili.

No comments