Plascon Yaahidi Kuwafikia Watanzania Wote, Yatoa Rangi kwa Kila Aina ya Mahitaji
Dar es Salaam.
Kampuni ya Plascon imeeleza kuwa imejipanga kuhakikisha bidhaa zake za rangi zinawafikia Watanzania katika maeneo mbalimbali nchini, huku ikitoa bidhaa zinazokidhi mahitaji ya ujenzi, magari, mbao, marine, chuma pamoja na matumizi ya ndani na nje ya nyumba.
Akizungumza katika Maonesho ya Samia Construction Awards yanayofanyika kwa siku nne kuanzia Jumanne hadi Ijumaa katika Kituo cha Mikutano cha Mlimani City, Dar es Salaam, Samuel Godfrey Maina, Mkuu wa Kitengo cha Ujenzi na Corporate wa Plascon, amesema kampuni hiyo imepanua mtandao wake wa matawi na depo ili kuhakikisha wateja wanapata huduma na bidhaa kwa urahisi.
Maina amesema Plascon inapatikana katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Dar es Salaam ambako ina makao makuu Tazara, pamoja na matawi ya Kamata na Salasala. Kampuni hiyo pia ina matawi Dodoma, Zanzibar, Mbeya, Arusha na Kahama.
Kwa upande wa kanda, amesema tawi la Mbeya linahudumia maeneo ya Mbeya, Iringa, Songea, Mbinga na sehemu mbalimbali za Ruvuma, huku tawi la Arusha likihudumia Arusha, Kilimanjaro, Tanga na maeneo ya jirani hadi Babati na Namanga.
“Tumelenga kuhakikisha tunafika kila sehemu ya nchi. Kwa mfano, tawi la Arusha linatuwezesha kufika hadi Namanga, wakati tawi la Mbeya linatusaidia kufikia maeneo yanayopakana na Zambia na Malawi,” amesema Maina.
Amesema upande wa Zanzibar, Plascon ina tawi linalohudumia visiwa vya Unguja na Pemba, huku tawi la Dodoma likihudumia Dodoma, Singida, Morogoro na baadhi ya maeneo ya Iringa, ikiwemo Mpwapwa.
Rangi kwa kila aina ya matumizi
Maina amesema Plascon ina bidhaa zinazolenga makundi mbalimbali ya watumiaji, kuanzia wateja wanaotafuta bidhaa za kiwango cha juu hadi wale wenye bajeti ndogo.
Ametaja miongoni mwa bidhaa hizo kuwa ni Silicon, ambayo amesema ni moja ya bidhaa za kiwango cha juu zinazotumika zaidi katika ulinzi wa kuta za nje ya majengo, pamoja na matumizi maalumu kama kwenye minara.
Pia ametaja Weatherguard, rangi inayolenga matumizi ya nje na iliyoundwa kustahimili mabadiliko mbalimbali ya hali ya hewa.
“Unaweza ukapaka Dar es Salaam ambako joto linaweza kufikia nyuzi 31 na ukapaka Mbeya ambako wakati mwingine halijoto hushuka sana, lakini bidhaa bado ikafanya kazi yake,” amesema.
Kwa matumizi ya ndani ya nyumba, amesema kampuni ina bidhaa kama Silk, huku Trade Wall Cover ikiwa chaguo kwa wateja wanaotafuta bidhaa yenye gharama nafuu zaidi.
Amesema pia Plascon ina High Cover Emulsion, ambayo inaweza kutumika katika nyumba za kupanga au majengo yanayohitaji bajeti ndogo ya upakaji rangi.
Suluhisho kwa mabati, magari na mbao
Katika sekta ya mabati, Maina amesema Plascon inaweza kumsaidia mteja anayehitaji kurejesha mwonekano wa bati zilizopauka kwa kumpatia rangi kulingana na hitaji lake.
Amesema wateja wanaweza kuchagua rangi mbalimbali, zikiwemo kijani, bluu, Dutch Blue au hata rangi maalumu ambayo inaweza kutengenezwa kulingana na mahitaji ya mteja.
Kwa upande wa magari, amesema kampuni ina bidhaa mbalimbali zinazohusisha rangi za magari, grill, plastiki, clear coat na polyurethane, ambazo zimeundwa kuhimili mazingira magumu yanayolikabili gari, ikiwemo jua, mvua na mabadiliko ya hali ya hewa.
Plascon pia ina bidhaa za kumalizia mbao, zikiwemo NC pamoja na bidhaa za Wood Care kwa matumizi ya ndani na nje.
“Tumezingatia kwamba mbao inayokaa nje inakabiliwa zaidi na jua na mazingira mengine kuliko mbao iliyoko ndani, ndiyo maana tuna bidhaa zinazolenga matumizi yote hayo,” amesema.
Rangi za marine na ulinzi wa chuma
Maina amesema kampuni hiyo pia ina kitengo maalumu cha rangi za marine, zinazotumika katika ulinzi wa boti na vifaa vinavyokabili mazingira yenye unyevu na chumvi.
Amesema bidhaa hizo zinaweza kutumika kwenye boti za kawaida pamoja na boti za uvuvi, ikiwemo maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria.
Kwa upande wa miundombinu ya chuma, amesema Plascon ina bidhaa za epoxy na primers zinazosaidia kulinda chuma dhidi ya kutu.
Ameeleza kuwa bidhaa hizo zimetumika katika miradi mbalimbali ya miundombinu, ikiwemo madaraja, kwa lengo la kuongeza ulinzi na uimara wa miundo ya chuma.
“Tumekuwa tukijaribu kuhakikisha tunafunika kila eneo. Sehemu ambayo hatuwezi kusema hatuna rangi ya kupaka ni chache sana. Plastiki tunaweza kupaka, chuma tunaweza kupaka na hata sehemu mbalimbali za magari ambazo zimetengenezwa kwa plastiki na fiber tuna bidhaa zake,” amesema.
Plascon yawalenga wafanyabiashara wadogo na wakubwa
Mbali na bidhaa, Maina amesema Plascon inatoa fursa kwa watu wanaotaka kuanzisha biashara ya rangi katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema kampuni ina mifumo tofauti ya kuwahudumia wafanyabiashara, ikiwemo akaunti za wateja wa kawaida, pamoja na mpango maalumu wa wafanyabiashara wanaotaka kuwa wauzaji wa kipekee wa bidhaa za Plascon.
Kwa wafanyabiashara wanaokidhi vigezo, amesema kampuni inaweza kuwapatia tinting machine bila malipo ya moja kwa moja, huku Plascon ikiendelea kumiliki mashine hiyo na kuwa na uwezo wa kuibadilishia programu inapohitajika.
Pia amesema kampuni ina huduma za mikopo kwa baadhi ya wateja wanaokidhi vigezo, ambapo wanaweza kupata bidhaa na kufanya malipo ndani ya siku 30.
“Tunao wateja wa cash, tunao wa credit na pia tunawaangalia wafanyabiashara wadogo ambao hawana mtaji mkubwa. Tunawapa ushauri kuhusu bidhaa gani wanaweza kuanza nazo ili ziweze kuzunguka na kumletea faida,” amesema.
Merchandising system yaongeza ajira
Maina amesema Plascon pia imeanzisha mfumo wa merchandising, ambapo kampuni inaweka wafanyakazi waliopatiwa mafunzo katika maduka ya baadhi ya wafanyabiashara ili kusaidia kuwaelimisha wateja kuhusu bidhaa.
Kwa mujibu wa Maina, wafanyakazi hao huwasaidia wateja kuelewa bidhaa zinazofaa kulingana na mahitaji yao, huku wakimsaidia mfanyabiashara kuongeza mauzo.
Amesema mfumo huo una manufaa kwa pande zote mbili kwa sababu unamsaidia mfanyabiashara kukuza biashara yake wakati huo huo Plascon ikiendelea kuajiri na kutoa fursa za ajira kwa Watanzania.
Plascon yajivunia miradi mbalimbali nchini
Maina amesema Plascon imehusika katika miradi mbalimbali ya ujenzi nchini kwa kusambaza rangi, huku baadhi ya majengo yaliyotumia bidhaa hizo yakiendelea kuonekana na kufanya vizuri hata baada ya miaka kadhaa.
Amesema kampuni hiyo inajivunia kuona baadhi ya majengo yaliyopakwa rangi zake miaka mingi iliyopita yakiendelea kuwa na mwonekano mzuri, licha ya kufanyiwa matengenezo ya kawaida.
“Plascon ni kampuni ambayo hata ukiwa huijatafuta, unaweza kukutana nayo. Unaweza kukutana na rangi zetu, mfanyakazi wetu au nyumba iliyopakwa rangi zetu. Tuna majengo mengi nchini ambayo tumesupply rangi na tunafurahi kuona hata jengo lililopakwa miaka 10 iliyopita likiwa bado linaonekana vizuri,” amesema.
Amesema ushiriki wa Plascon katika Samia Construction Awards ni sehemu ya jitihada za kampuni kuendelea kuwa karibu na wadau wa sekta ya ujenzi, kuonesha bidhaa zake na kueleza namna inavyoweza kutoa suluhisho kwa mahitaji mbalimbali ya ujenzi na sekta nyingine.
Samuel Godfrey Maina ni Mkuu wa Kitengo cha Ujenzi na Corporate wa Plascon.

Post a Comment