KATAMBI: HAKUNA MUHALIFU ATAKAYEJIFICHA NJE YA NCHI, JINAI HAIOZI
Katambi amesema Serikali inaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya uhalifu kupitia makubaliano mbalimbali ya nchi kwa nchi, ikiwemo mikataba ya kurejeshana wahalifu (extradition) na ushirikiano wa kisheria katika masuala ya jinai.
Amesema kutokana na ushirikiano huo, mtuhumiwa au mhalifu anayekimbilia nchi ambayo Tanzania ina makubaliano nayo hawezi kudhani kuwa yuko salama, kwa kuwa vyombo vya dola vinaweza kumfuatilia na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.
“Hakuna muhalifu ambaye yuko nchi fulani ambayo tumeingia nayo makubaliano atabaki kuwa salama. Ni suala la muda tu,” alisema Katambi.
Waziri huyo pia amelitaja Jeshi la Polisi kuwa miongoni mwa taasisi zinazotekeleza wajibu huo, akilitaja chini ya uongozi wa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Camillus Wambura.
Akizungumzia utekelezaji wa sheria, Katambi amesema hakuna mtu anayepaswa kuamini kuwa umaarufu, utajiri, cheo au kuwa na ukaribu na viongozi kunaweza kumkinga dhidi ya makosa ya jinai.
Amesisitiza kuwa hata yeye mwenyewe kama Waziri wa Mambo ya Ndani hayuko juu ya sheria, akibainisha kuwa msimamo wa Serikali ni kuhakikisha haki inapatikana bila kujali hadhi au nafasi ya mtu.
“Hakuna mtu aliye juu ya sheria. Hata mimi Waziri wa Mambo ya Ndani siko juu ya sheria,” amesema.
Katambi amesema Serikali haitaki kuona watu wakiviziana au kupendeleana katika utekelezaji wa sheria, bali kila mmoja anatakiwa kuwajibika kwa matendo yake kwa mujibu wa Katiba, sheria, taratibu na kanuni.
AWAONYA WANAOTUMIA MITANDAO KUTAFUTA ‘VIEWS’
Waziri huyo ametoa pia rai kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii, wasanii na watengeneza maudhui kuacha kuzalisha maudhui yenye lengo la kupata watazamaji (views) au mapato bila kuzingatia madhara yanayoweza kuikumba jamii.
Amesema baadhi ya maudhui yanaweza kudhalilisha utu na heshima ya watu, kuleta migawanyiko katika jamii na kuwa na athari kwa watoto na kizazi kijacho.
Kwa mujibu wa Katambi, kujenga heshima na hadhi ya mtu ni mchakato unaoweza kuchukua miaka mingi, lakini inaweza kuharibiwa kwa tukio moja au maudhui moja yanayosambaa kwa kasi mitandaoni.
“Ujenzi wa heshima na hadhi ni uwekezaji wa muda mrefu, lakini kubomoka ni kwa siku moja. Kujenga ni kugumu zaidi kuliko kubomoa,” amesema.
Amesema Serikali haitaki kuona umaarufu wa mtu ukitumika kama sababu ya kufanya makosa ya jinai au kuvunja haki za wengine.
RAI KWA VYOMBO VYA HABARI
Katambi pia amewataka wamiliki wa vyombo vya habari na wanahabari kuzingatia sheria na maadili katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema ingawa sekta ya habari ina mamlaka na taasisi zinazosimamia shughuli zake, baadhi ya vitendo vinavyofanywa katika tasnia hiyo vinaweza kuvuka mipaka ya masuala ya kitaaluma na kuingia katika makosa ya jinai.
Ameeleza kuwa Serikali ina wajibu wa kikatiba wa kusimamia usalama na ustawi wa wananchi, hivyo haitoweza kupuuza vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama au ustawi wa jamii.
Waziri amesema tayari kumekuwa na mawasiliano na viongozi wenye dhamana ya habari, maadili, mawasiliano na taasisi nyingine zinazohusika, kwa lengo la kuhakikisha kila mamlaka inatekeleza wajibu wake katika eneo lake.
“TUMETOA ELIMU, MSISEME HAMJAAMBIWA”
Katambi amesema Serikali imechukua hatua ya kutoa elimu kwa umma kabla ya kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wanaokiuka sheria.
Amesema baada ya elimu hiyo, mtu atakayekiuka sheria hatapaswa kutarajia kupewa upendeleo kwa sababu ya cheo, fedha, umaarufu au nafasi yake katika jamii.
“Tutachukua hatua kwa sababu msiseme hamjaambiwa. Tumetekeleza wajibu wetu tena wa ziada sana. Kutokujua sheria sio kinga,” amesema.
Amesema elimu hiyo itaendelea kutolewa kupitia taasisi mbalimbali za Serikali, ikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama, huku viongozi na taasisi wakifika katika maeneo mbalimbali ya jamii ili kuwafikia wananchi moja kwa moja.
Katambi amesema lengo si kuwatisha wananchi bali kuhakikisha kila mtu anafahamu mipaka ya matumizi ya mitandao, anaheshimu haki za wengine na anaelewa kuwa sheria zinamhusu kila mtu bila kujali umaarufu au nafasi yake.
“Tusilibomoe taifa letu. Tusibomoe hadhi, heshima na utu wa mtu,” amesisitiza.

Post a Comment